MALALAMIKO YA WANANCHI KUHUSU HUDUMA DUNI ZA TANESCO ZASABABISHA DC JOKATE KUWAWEKA NDANI BAADHI YA WATENDAJI, ATOA NENO KWA TAKUKURU | Tarimo Blog

Na Said Mwishehe,Michuzi TV .

MKUU wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Jokate Mwegelo ameamuru kuwaweka ndani baadhi ya watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO) katika wilaya hiyo baada ya kukithiri kwa malalamiko ya huduma duni ya nishati ya umeme kwa wananchi.

Jokate amefikia uamuzi huo baada ya k
ufanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za TANESCO Wilaya Kisarawe kuona namna ambavyo huduma zinatolewa na baada ya kufika hapo alikutana na idadi kubwa ya wananchi ambao wamefika kutoa malalamiko yao kutokana na kukosa huduma ya nishati ya umeme kwa wakati.

Akizungumza akiwa katika ofisi hizo za TANESCO, Jokate amesema hawezi kukubali kuona wananchi wakiendelea kulalamika kuhusu nishati ya umeme na kibaya zaidi baadhi ya watendaji wamekuwa wakiwapuuza na kuwadharau wananchi wanaofika kuhitahi huduma mbalimbali za shirika hilo.
"Haiwezekani wananchi wawe wanalalamika kila siku kuhusu huduma za TANESCO hapa Kisarawe, tumekuwa tukizungumza mara nyingi kwenye vikao vyetu , lakini ninyi wenzetu hamtaki kusikia wala hamfanyii kazi malalamiko ya wananchi.

"Sasa niwaambie mimi niko na wananchi, malalamiko ni mengi, tunakubaliana na humfanyi kazi , nachukua haya malalamiko na kuyafikisha kwa Mtendaji Mkuu wa TANESCO maana ninyi hapa mmeshindwa kuyafanyia kazi, huduma kwa wateja mbovu.

"Katika kipindi ambacho Serikali imedhamiria kuboresha sekta ya nishati haya ambayo yanaendelea hapa kwetu hayapaswi kuwepo, hatuwezi kuendelea hivi.Kuna maeneo kwa siku umeme unakatika zaidi ya mara tano, wananchi wanatoa taarifa hazifanyiwi kazi kwasababu tu umeamua kuwapuuza,"amesema.

Jokate ameongeza  kuna kiongozi wake yupo karibu kabisa na TANESCO na alipata tatizo la hitilifu ya umeme kwenye nyumba yake lakini ilichukua zaidi ya mwezi mmoja hakuna huduma aliyopatiwa.
"Shida ya hapa ni nini? Wananchi wako wengi na wote wanalalamikia TANESCO,Meneja  kaa na timu yako muondoe kero za wananchi, kesho asubuhi nataka nipate taarifa jinsi ambavyo mmeshughulikia hizi kero zote na wote walioko hapa nataka wapate huduma leo leo, mtafanyaje mtajua wenyewe,"amesisitiza.

Aidha amesema sababu kubwa ya kuwepo kwa malalamiko mengi ya wananchi inatokana na kukithiri kwa vitendo vya rushwa kwa baadhi ya watendaji na watumishi wa TANESCO."Kuna watendaji wanapenda rushwa na matokeo yake wanakwamisha huduma kupatikana kwa wakati unaotakiwa."amesema Jokate huku akitoa amri ya Polisi kukamatwa kwa baadhi ya watendaji na watumishi wa shirika hilo ili wakae rumande wajitafakari wakiwa huko.

"Wanaohusika wote na kutoa huduma kwa wateja wapelekwe kituo cha Polisi watafakari utendaji wao wa kazi na maisha yao.Wamekuwa na dharau na wala hawawaheshimu hawaheshimu mammlaka, na wananchi, hawaheshimu mamlaka na unapowadharau wananchi maana yake unamdharau hadi Rais,"amesisitiza.

Hata hivyo amesema kuna haja ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) kufanya uchunguzi katika ofisi za TANESCO Kisarawe ili kukomesha rushwa ambazo zinatolewa kwa baadhi ya watumishi wa shirika hilo.

"TANESCO inabidi tutalalamike tukikosa wateja, lakini wateja wote hawa bado tunaona ni mzigo.DAWASA wanapata shida? Mbona hawapati shida na ni wapya? Hawa wananchi ndio hazina yenu, hakikisheni kero zao zinapata majibu, mnawakosea sana na mnawanyima haki zao.

"Mwananchi yoyote akichukuliwa poa maana yake umenichukulia poa mimi, haikubali, kama nilivyotangulia kueleza tumeitana mara nyingi na tumezungumza kwenye vikao lakini hakuna kinachofanyika , mmesababisha tufike hapa ambapo leo tumefika.Acheni kuwa na tamaa ndogo ndogo na niwaambie Rais akija hapa mtambuliwa ndani ya dakika mbili tu,"amesisitiza Jakate.

Akizungumza mbele ya DC Jokate, Mhandisi Nickson Babu ambaye ni Meneja wa TANESCO Chanika amekiri kuwepo kwa changamoto hizo lakini wameahidi kuzifanyia kazi mara moja huku akieleza shirika hilo limeendelea kusogeza huduma karibu na wananchi ikiwemo ofisi ya Chanika."Tunaahidi kufanyia kazi yale yote ambayo Mkuu wa Wilaya ameyatolea maelekezo kwetu."

 

 MKUU wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Jokate Mwegelo


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2