WANAOWATUMIKISHA WALEMAVU KUOMBAOMBA JIJINI DAR ES SALAAM KIZIMBANI | Tarimo Blog


Wafanyabiashara Sadikiel Meta 15 wakiwa wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 41 yakiwemo ya kuwatumikisha walemavu na kuwafanya kuwa ombaomba jijini Dar es Salaam.

MFANYABIASHARA Sadikiel Meta mwenye umri wa miaka 71 na wenzake 14 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 41 yakiwemo ya kuwatumikisha walemavu na kuwafanya kuwa ombaomba.

Mengine ni usafirishaji haramu wa binadamu, kutakatisha fedha,  kukwepa kulipa kodi na ba kuisababishia serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasara ya zaidi ya sh. Milioni 31.3

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa serikali Mwandamizi Mkunde Mshanga akisaidiana na Wankyo Simon imewataja washtakiwa wengine kuwa ni Yusuph Mohamed (35), Yusuph Magadu (20), Emmanuel Salu (20) Gogad Mayenga (18), Samson Taruse (26), Hussein John (18), Zacharia Paul (18), Dotto Shigula (19), Petro Simon (21), Emmanuel Sahani (38), Joseph Mathias (20), Masanja Paul (21), Aminiel Sangu (19), na Emmanuel Lusinge.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Kassian Matembele imedaiwa katika tarehe tofauti za Agosti 2020 na Januari Mosi 2021 jijini Dar es Salaam,  Washtakiwa wote kwa pamoja walishiriki kufanya uhalifu wa kupanga kwa kuongoza genge la uhalifu na kutekeleza kufanikisha kusafirisha binadamu kwa haramu.

Katika shtaka la pili la usafirishaji haramu wa binadamu inadaiwa, katika kipindi hicho hicho huko Tandale ndani ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam mshtakiwa Meta na Mohamed waliwatumikisha walemavu 37 na kuwafanya wawe ombaomba wa mtaani kwa lengo la kujipatia kipato.

Miongoni mwa wa walemavu hao ni mtoto Kashinje Emmanuel,  mwenye umri wa miaka saba, Doto Silas Happines Bezagurwa, Neema Edward na  Peter Sereke wote wa ama umri wa miaka 11.

Imedaiwa wa washtakiwa hao pia walikuwa wakisafirisha walemavu kutoka mikoa ya Shinyanga na Tabora kwenda Dar es Salaam na kwamba wakishapokelewa wanawaingiza kwenye shughuli za ombaomba kwa lengo la kujipatia faida.

Aidha mshtakiwa Meta anadaiwa kushindwa kulipa kodi ya thamani ya Sh. 31,328,500.31 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) .

Pia mshtakiwa Meta anadaiwa kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh. Milioni 31.3.

Katika shtaka la mwisho la utakatishaji imedaiwa kati ya Agosti 2020 na Januari Mosi 2021, mshtakiwa Meta alijipatia Sh. Milioni 31,328,500.31 huku akijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la kushindwa kulipa kodi.

Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu  kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na kesi imeahirishwa hadi Januari 26,2021.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2