MOROGORO YAJIPANGA KUKUZA UZALISHAJI WA ZAO LA MAHINDI | Tarimo Blog

 

 Wito umetolewa kwa maafisa ugani mkoani Morogoro kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula hususani zao la Mahindi.
 
 Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare wakati wa halfa ya kukabidhi pikipiki 10 zilizotolewa na Serikali ya China na serikali ya Mkoa wa Morogoro kwa maafisa ugani 10 kati ya 42 waliofanya vizuri katika utekelezaji wa Mradi wa kukuza kilimo cha zao la mahindi mkoani Morogoro, mradi una
otekelezwa  kwa ushirikiano kati ya  Chuo Kikuu cha Kilimo cha China na Serikali ya Mkoa wa Morogoro huku ukisimamiwa na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
 
 Akizungumza katika hafla hiyo, Sanare alisema kuwa mkoa wa Morogoro una ardhi kubwa na nzuri ifaayo kwa kilimo cha mazao ya aina mbali mbali ikiwemo mahindi lakini uzalishaji wa zao hilo uko chini kulinganisha na ubora wa ardhi ya mkoa huo.

 “ Mradi huu wa kukuza kilimo cha  zao la mahindi, umeonesha tija na ninatumai kuwa utakuwa na tija kubwaza zaidi katika kukuza uzalishaji wa zao hili muhimu la chakula. Ni wakati sasa maafisa ugani  kumuunga mkono kwa vitendo Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli, kuchapa kazi kwa bidii, kutoka ofisi na kwenda kwa wakulima kuwafundisha njia bora za uzalishaji wa zao hili ili wazalishe kwa wingi”
 
 Sanare aliongeza kusema kuwa pikipiki walizopewa maafisa ugani hao ziwe chachu ya kufanya kazi kwa bidii kwa kuwafikia wakulima mashambani mwao na kuwapatia utaalamu wa kuzalisha kwa tija. Aliwaasa maafisa ugani hao kutotumia pikipiki hizo kwa shughuli binafsi kinyume na malengo yanayo tarajiwa ambayo ni kuwafikiwa wakulima kwa wakati.
 
Akitoa taarifa ya mradi mradi huo wa kukuza uzalishaji wa kilimo cha zao la mahindi, Mratibu wa mradi, Ernest Mkongo, alisema kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2013 katika vijiji viwili na baadae kufikia vijiji 10 huku ukiwa umeonesha mafanikio makubwa.
 
“Mradi huu unatarajiwa kufikia ukomo mwaka huu wa 2021, ambapo zaidi ya wakulima 2000 wamefikiwa moja kwa moja. Ni matarajio yetu kuwa  idadi hiyo ya wakulima itaongezeka kwa haraka kwani tunao wataalamu wa kutosha wenye nyezo za kuweza kulifikia kundi kubwa zaidi la wakulima mkoani hapa.” Alisema Mkongo.

Naye Afisa Ugani wa kijiji cha Mtego wa Simba,Halmashauli ya Morogoro, moja ya kijiji kinachotekeleza mradi huo Veronica Lugano, alisema kuwa kabla ya mradi huo wakulima walikuwa katika kijiji chake wakizalisha kati ya gunia 2 mpaka 3 kwa hekali moja, kwa sasa wakulima hao wanazalisha kati ya gunia 10 mpaka 20 kwa hekali moja.
 
 Lugano alisema kuwa ana matumaini makubwa kuwa tenkolojia hiyo ya kukuza uzalishaji wa zao la mahindi ikiwa itatumiwa vizuri na wakulima itaufanya mkoa wa Morogoro kuzalishaji zao la mahindi kwa wingi.
 
 Alisema kuwa maafisa ugani wamejipanga kusimamia kikamilifu uzalishaji wa zao hilo mkoani Morogoro kwa kuhamasisha na kuwafundisha wakulima kulima kilimo cha kisasa kwa kutumia kanuni bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwa ajili ya kukuza uchumi wa mkoa wa Morogoro na Taifa kwa ujumla.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2