Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya akizungumza
jambo katika mkutano na wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu ya
Handali yaliopo Chamwino Mkoani Dodoma.
Baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini dhahabu wa Handali
yaliopo Chamwino Mkoani Dodoma walioshiriki Mkutano na Naibu Waziri wa
Madini Prof. Shukrani Manya.
Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya akisaini
kitabu cha wageni katika Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha
Handali.
Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya akijadili jambo
na baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika mgodi wa
Handali yaliopo Chamwino Mkoani Dodoma.
Na Tito Mselem, Dodoma
DHANA ya Serikali kufanya mabadiliko ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010
na Marekebisho yake ya Mwaka 2017 ni kuwawezesha wachimbaji wadogo wa
madini kuchimba kwa tija na kuzalisha kwa faida.
Kauli hiyo, ameitoa Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya
alipotembelea Mgodi wa Handali uliopo Wilaya ya Chamwino jijini Dodoma
ambapo alizungumza na kutatua kero za wachimbaji wadogo katika Mgodi
huo.
Imeelezwa kuwa Mgodi wa Handali ulianza miezi sita iliyopita na
ulianza kama mlipuko wa madini ya dhahabu (Rush), ambapo mpaka sasa
una mialo 28 kalasha 30 na umeweza kuvuna dhahabu ya Uzito wa Gramu
816.77 yenye thamani ya Shilingi 89,293,000/- na dhahabu inayopatikana
eneo hilo ina kiwango cha ubora cha asilimia 80.
Aidha, Prof. Manya amesema, Shughuli za madini zimeimarishwa ambapo
kila Mkoa kuna Afisa Madini Mkazi ambaye yupo eneo husika kwa ajili ya
kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini wa Mkoa husika.
“Niwaombe wachimbaji wadogo wa madini kote nchini kuzitumia Ofisi za
Maofisa Madini Wakazi katika maeneo yenu ili wawape ufafanuzi wa
changamoto yoyote katika maeneo yenu na myatumie Masoko ya Madini
yaliopo sehemu mbalimbali nchini kuuzia na kununulia madini yenu na
kwa yoyote atakaye kiuka atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo
kufilisiwa, faini, kwenda jela, au kufutiwa leseni na kuzuiliwa
kujihusiha na shughuli yoyote inayohusiana na Madini,” alisema Prof
Manya.
Pia, Prof. Manya amewataka wachimbaji wadogo wa madini nchini
kupendana, kushirikiana, kuthaminiana na kuachana na wivu, fitina na
majungu ili wafanye shughuli zao kwa tija ambapo mpaka sasa Serikali
imewawekea mazingira wezeshi wachimbaji wadogo na kuimarisha
ushirikiano kati ya Wizara ya Madini na Mikoa, Wilaya mpaka kwenye
ngazi ya Vijiji katika shughuli za madini.
Vile vile, Prof Manya amemuagiza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma
Nchangwa Marwa kutoa elimu ya Uchimbaji Salama kwa wachimbaji wadogo
katika mgodi huo, ambapo alisema hayo kutokana na mvua za masika
zinazoendelea kunyesha nchini kote.
Katika hatua nyingine, Prof. Manya, amewataka madalali wote wa madini
(Brocker) kuhakikisha wanafanya biashara na wawe na leseni za biashara
ya madini ambaye hana alielekezwa amuone Afisa Madini Mkazi wa Mkoa
huo.
Naye, Mkuu wa Wilaya Chamwino Vumilia Chamiga alimshukuru Prof. Manya
kwa kusikiliza na kuzitatua kero za wachimbaji wadogo wa Mgodi huo na
kuahidi kwamba atashirikiana na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa
Dodoma ili watoe elimu ya Uchimbaji Salama hasa katika kipindi hiki
cha mvua.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment