Na Ramadhani Ali -Maelezo
WIZARA ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda imeahidi kuendelea kushirikiana na kuwaendeleza wabunifu ili waweze kukua na hatimaye kujiajiri wenyewe kupitia ubunifu wao.
Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Juma Reli ameeleza hayo katika siku maalumu ya ubunifu ndani ya Tamasha la saba la Biashara linalofanyika Viwanja vya Maisara.
Amesema Wizara imeandaa siku siku hiyo ndani ya Tamasha la Biashara, linalofanyika kila mwaka, ikiwa ni miongoni shamra shamra za maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar, ili kutoa nafasi kwa wabunifu kuonyesha vipaji vyao.
Aliwashauri wabunifu wa Zanzibar kutumia Taasisi za fedha zilizopo nchini katika kuimarisha ubunifu na vipaji vyao kwani ni sehemu ya kuleta Mapinduzi ndani ya nchi.
Katibu Mkuu alieleza kuwa kwa kawaida ubunifu unatoa nafasi ya kubadilisha Teknolojia ya zamani na kuingia katika Teknolojia ya kisasa ya kisayansi ambayo inapunguza gharama na muda na kuongeza ufanisi.
Aliwapongeza washiriki wote wa mashindano ya ubunifu na kusisitiza kuwa iwapo ubunifu utatumika vizuri unanafasi kubwa ya kusaidia kuinua maisha yao na kukuza uchumi wa nchi.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Viwanda vidogo vidogo na vya kati (SMIDA) Haji Abdulhamid alisema lengo la kuandaa siku maalum ya Ubunifu katika kipindi cha Tamasha la Biashara ni kujaribu kutatua baadhi ya matatizo kupitia ubunifu unaofanywa.
Ameishauri jamii kuwapa moyo na kuwasaidia wabunifu ili waweze kutekeleza kazi zao ambazo ni muhimu katika kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Juma Reli aliwakabidhi vyeti na fedha taslimu washindi watatu wa mwanzo katika mashindano ya ubunifu wa mashine na ICT ambapo jumla ya wabunifu 20 walishiriki mashindano hayo.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment