Na Nelson Kessy, Chato
Mjumbe wa Baraza la Taifa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamuhuri ya Watu wa China, mhe. Wangi Yi ameanza ziara yake ya kikazi ya kikazi nchini Tanzania.
Mhe. Wangi Yi amewasili majira ya saa 11 jioni katika uwanja wa ndege wa Geita - Chato na kupokelewa na mwenyeji wake Mhe. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi, (Mb).
Mara baada ya kuwasili, Mhe. Wang Yi ameshiriki katika uzinduzi wa chuo cha Veta kilichopo Chato mkoani Geita, ambapo ujenzi wa chuo hicho umegharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza wakati akimkaribisha Mhe. Wang Yi katika uzinduzi wa chuo hicho, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka umuhimu mkubwa katika Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, ili kufanikisha kujenga uchumi wa viwanda, na kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025.
"Lengo letu ni kujenga angalau kituo kimoja cha umma cha mafunzo ya ufundi stadi katika kila wilaya," amesema Prof. Ndalichako
Aidha, Prof. Ndalichako ameongeza kuwa lengo kubwa la Serikali ni kujenga vyuo vingi vya Veta kwa kutumia vyanzo vya mapato vya ndani na kwa ushirikiano na mataifa rafiki ambapo mpaka sasa Serikali ina vituo 41 vya umma vya mafunzo ya ufundi stadi nchini na vingine 29 vinaendelea kujengwa.
Pia Prof. Ndalichako amesema Serikali ya Tanzania iko tayari kupokea moja ya kati ya karakana 10 za mafunzo za Luban (Luban Workshops), ambazo China imedhamiria kuzijenga barani Afrika, ili kutoa mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana wa ki-afrika. Karakana hiyo inaweza kuwa sehemu ya Kituo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chato ambacho tumekizindua leo.
Kwa upande wake Mjumbe wa Baraza la Taifa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Wang Yi, amesema ili Taifa lolote liweze kupiga hatua za na kiteknolojia na kufikia malengo ya mapinduzi ya viwanda ni lazima taifa hilo liwe na vijana wenye ujuzi wa kitaaluma hivyo chuo cha Veta ni mojawapo ya maeneo ya kuwajengea vijana uwezo wa kitaaluma.
Mhe. Wang Yi ameongeza kuwa Serikali ya China ipo pamoja na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha vijana wanapata mafunzo ya kitaaluma katika vyuo vya Veta na kwa kudhihirisha hilo, China inachangia kiasi cha RB 1,000,000 za China sawa na fedha za kitanzania Shilingi 350 milioni kwa ajili ya kuendeleza chuo cha Veta - Chato.
"Binafsi naomba kumpongeza Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwa mwanamapinduzi wa kweli kiuchumi na kitaaluma ambapo amefanikiwa kujenga idadi kubwa ya vyuo vya ufundi ili kuwajengea vijana uwezo wa kitaaluma jambo ambalo litachangia mapinduzi ya kiuchumi," Amesema Wang Yi.
China inasaidia Tanzania chuo cha VETA mkoani Kagera ambacho kina uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,000 ambapo ujenzi wake unaendelea.
Mjumbe wa Baraza la Taifa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamuhuri ya Watu wa China, mhe. Wangi Yi akimkabidhi Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako kiasi cha Shilingi milioni 350 kwa ajili ya kuendeleza chuo cha VETA. Chuo hicho kimejengwa kwa fedha za Serikali ya Tanzania.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako pamoja na Mjumbe wa Baraza la Taifa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamuhuri ya Watu wa China, mhe. Wangi Yi wakizindua chuo cha VETA
Makatibu Wakuu, Mabalozi na viongozi waandamizi wa Serikali wakishuhudia uzinduzi wa chuo cha VETA Chato leo Mkoani Geita .
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment