Na Mwandishi Wetu, Chato
WAZIRI wa Mambo ya Nje ya China, Wang Yi amewasili nchini Tanzania kwa ziara ya siku mbili ambapo pamoja na mambo mengine leo Januari 7,2021 amezindua Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) wilayani Chato mkoani Geita.
Mbali ya kuzindua chuo hicho ametoa msaada wa zaidi ya Sh.milioni 350 ambazo zitatumika katika Chuo hicho kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya mafunzo ya uvuvi kwa wananchi wa Wilayani Chato.
Akizungumza leo baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege Chato mkoani Geita nchini na kupokelewa na Viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi pamoja na Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Waziri Wang Yi amesema Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China itaendelea kusaidia vyuo vya ufundi nchini.
Hivyo amesema katika kuendeleza jitihada hizo ametoa fedha za China Yuan milioni moja ambazo ni sawa na Sh.milioni 350 za Kitanzania kwa ajili ya kusaidia Chuo cha VETA- Chato hasa katika kusaidia fani ya uvuvi kutokana na wilaya ya Chato kuwa wananchi wengi wanaojihusisha na uvuvi, na hivyo kupitia Chuo hicho Wananchi hao watapatiwa mafunzo.
"Balozi wa China nchini Tanzania atakuwa hapa kwa ajili ya kuhakikisha Chuo hiki ambacho tumekizindua kinasonga mbele. China inaona fahari kubwa kusaidia Vyuo vya Ufundi Stadi vya Tanzania na siku za karibuni imesaidia ujenzi wa Chuo cha VETA Kagera na hata kule Dodoma. Hapa ninaona kuna Mabinti na Wavulana wengi na wanahitaji kuendelezwa kwa ajili ya kuisadia nchi yao,"amesema Waziri Wang Yi.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amesema fedha ambazo zimetolewa na kukabidhiwa kwake kwa niaba ya Serikali ya Tanzania ambazo ni Yuan Milioni moja sawa Sh.milioni 350 na zitatumika katika Chuo hicho na hasa katika ununuzi wa vifaa vya mafunzo ya fani ya uvuvi.
Awali akikamkaribisha Waziri Wang Yi baada ya kuzinduliwa kwa Chuo hicho, Profesa Ndalichako amesema wanayo furaha kubwa kuijumuisha Tanzania katika ziara yake hiyo kwa nchi za Afrika. "Umezindua Chuo cha VETA wilayani Chato na hii inaonesha uhusiano madhubuti uliopo baina ya nchi hizi mbili.
"Mheshimiwa Waziri Wang Yi, Serikali yetu imeweka umuhimu mkubwa katika elimu ya ufundi na mafunzo stadi ili kufikia malengo ya Serikali na mkakati wetu ni kujenga Chuo cha VETA katika kila Wilaya kwa mwaka 2025. Tunaamini tutafanikiwa katika ujenzi wa vyuo hivyo kupitia vyanzo vyetu vya ndani pamoja na ushirikiano wa wadau wa maendeleo ikiwemo Jamhuri ya Watu wa China. Kwa sasa tunavyo vituo vya VETA 41.
"Sasa niruhusu kuwasilisha shukrani za Tanzania kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kujenga Chuo cha VETA mkoani Kagera, tunatarajia misaada zaidi katika kujenga vituo vingi zaidi nchini chini ya mpango wa kujenga uwezo kati ya Tanzania na China.
"Tunatarajia kupata wakufunzi wa mafunzo ya ufundi stadi kutoka China pamoja na kupanua ushirikiano wa mafunzo ya ufundi stadi katika nchi hizo mbili, na tunaomba taasisi za China ambazo zipo hapa Tanzania kufanya kazi pamoja na VETA.
"Tunaamini tutakuwa na ushirikiano unaonufaisha pande zote mbili kupitia mafuzo ya ufundi stadi ambayo ni njia ya uhakika wa maendeleo yanayojitegemea. Kwa mara nyingine nakushukuru sana kwa kukubali kuzindua Chuo cha VETA -Chato na nchi yako kuendelea kusaidia Tanzania,"amesema Waziri Ndalichako.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment