Na Mwandishi wetu, Simanjiro
HALMASHAURI ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, imefanikiwa kupata sh270 milioni baada ya kufanikisha ukamilishaji wa miradi sita ya maji na usafi wa mazingira mashuleni.(Swash).
Halmashauri hiyo imefanikiwa kuwa ya kwanza mkoani Manyara, kati ya halmashauri saba kwani imeongoza kwenye miradi sita miongoni mwa miradi saba iliyotolewa kwa kila halmashauri hizo.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Yefred Myenzi akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani, amewapongeza wataalamu, madiwani na kamati zilizosimamia miradi hiyo.
Myenzi amesema baada ya halmashauri ya wilaya ya Simanjiro kuongoza kwenye mkoa wa Manyara, itapatiwa fedha hizo sh270 milioni ili kufanikisha miradi mingine.
Amesema hiyo ni hatua kubwa kwani halmashauri nyingine hazikukamikisha miradi hiyo kwa wakati ndiyo sababu wao wakaongoza kwa kukamilisha miradi sita kati ya saba.
"Mkuu wa mkoa wa Manyara, Joseph Mkirikiti alitembelea moja kati ya miradi hiyo hapa Simanjiro kwenye eneo la Ngage na kuagiza wenzetu wengine waje waige mfano hapa kwetu ubora wa miradi," amesema Myenzi.
Amesema fedha hizo kutoka kwa wafadhili zitachangia kufanikisha miradi mingine ili kuhakikisha wanaondokana na magonjwa ya milipuko kutokana na hali ya usafi uliopo.
"Hivi sasa tunataka magonjwa yote ya milipuko ikiwemo kipindupindu inakuwa historia kutokana na hali ya usafi wa mazingira na kuwepo kwa vyoo," amesema Myenzi.
Amesema fedha zilizotengwa kwenye miradi hiyo zilitumika ipasavyo katika usafi wa mazingira, uboreshaji wa maji na ujenzi wa vyoo ili kuondokana na maradhi.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga amempongeza Myenzi kwa namna anavyosimamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
"Mkurugenzi wetu Myenzi tunapaswa kumpongeza kwani amekuwa kiranja wa kusimamia miradi ya maendeleo ipasavyo hivyo tumuunge mkono kwa maslahi mapana ya wana Simanjiro," amesema Kanunga.
Hata hivyo, amesema anashukuru ushirikiano anaoupata kupitia mkuu wa wilaya hiyo, mhandisi Zephania Chaula, Katibu Tawala, Zuwena Omary, mbunge wa Jimbo Christopher Ole Sendeka na Mkurugenzi Myenzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Yefred Myenzi akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani, kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Baraka Kanunga Laizer na Katibu Tawala Zuwena Omary Jiri
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment