COSOTA na BASATA zaagizwa kukamilisha Mfumo wa uuzaji kazi za Sanaa Mtandaoni | Tarimo Blog

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa akitoa maelekezo kwa COSOTA na BASATA kuandaa mfumo wa kuuza kazi za Wachoraji na Wachongaji kwa njia ya mtandao kufuatia ukuaji wa teknolojia na uwanda mpana wa masoko katika mfumo wa mtandao au programu za simu ’Apps’ leo Machi 15,2021 Jijini Dar es Salaam katika kikao wadau wa Sanaa ya Uchoraji na Uchongaji kilicholenga kutatua changamoto zinazowakabili.

Na Richard Mwamakafu – WHUSM
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa ameiagiza COSOTA na BASATA kuandaa mfumo utakaosadia wasanii kuuza kazi zao mtandaoni.

Mhe.Bashungwa ameyasema hayo Machi 15, 2021 alipokutana na Chama cha Wasanii Wachongaji Tanzania (CHAWASAWATA) na Uchoraji (Tingatinga) ili kujua na kujadili Changamoto zinazowakabili ambapo ameahidi kuzifanyia kazi.

"Inabidi kushirikiana na vyama hivi ili kutengeneza platform ya mitandaoni ili kuuza bidhaa lakini nakulinda kazi za wasanii hawa, tuliahidi kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi kuanzisha mfuko wa sanaa na kwa habari iliyo njema kwa maelekezo ya Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli mfuko huu umeuwishwa sasa tunaanza kuutengea fedha kwa Mwaka huu wa Fedha 2021/2022 ambayo Bunge litakaa kwaajili yakuijadili hiyo bajeti lakini matarajio yetu kuanzia mwezi Julai angalau huu Mfuko uanze kuwa na Fedha kwaajili yakutoa mkopo kwa Wasanii wetu" alisema Mhe.Bashungwa.

Mheshimiwa Bashungwa aliwahakikishia wasanii hao kuwa serikali iko nao bega kwa bega katika kuisimamia sekta hiyo ya sanaa na kuahidi kuwa serikali ipo tayari kusikiliza na kutoa ushirikiano.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki Tanzania (COSOTA) Bibi.Doreen Sinare alieleza kuwa taasisi hiyo imetengeneza Kanuni mpya ambazo zitawasaidia

Wachoraji na Wachongaji kunufaika na kazi zao baada ya kuuza kazi hizo nje ya nchi kupitia minada na njia nyingine ambapo kazi huuzwa kwa bei za juu ilihali msanii kutokupata chochote kutokana na mauzo hayo zijulikanazo kama ‘resale royalties rights’.

Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) Bw.Matiko Mniko alieleza kuwa Baraza katika kutatua changamoto ya Masoko kwa Wasanii wa Sanaa ya Ufundi wameanzisha Kampeni ambayo itashirikisha taasisi mbalimbali kuanzisha minada ambayo itakuwa ikifanyika Dodoma na Dar es Salaam angalau mara mbili kwa mwaka.


Mkutano huo uliratibiwa na BASATA chini ya Kaimu Mtendaji Matiko Mniko na kuhudhuriwa na Rais wa Shilikisho la Sanaa za Ufundi Adrian Nyangamale, pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu COSOTA Bibi m Doreen Sinare na mwakilishi wa Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa (WHUSM) Bw.Habibi Msami.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2