VIUMBE VYA BAHARINI 100,000 HUFA KILA MWAKA KWA SABABU YA TAKA ZA PLASTIKI | Tarimo Blog

 VIUMBE VYA BAHARINI 100,000 WANAKUFA KILA MWAKA KWA SABABU YA TAKA ZA PLASTIKI

Charles James, Michuzi TV

VIUMBE vya baharini zaidi 100,000 wanakufa kila mwaka kwa sababu ya uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na bidhaa za plastiki zinazotupwa baharini.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani, Dk John Mduma, wakati akihitimisha maadhimisho ya siku ya Haki za Mlaji Duniani.

Amesema takwimu hizo ni matokeo ya utafiti uliofanywa mwaka juzi na mtandao wa Consumers International kuhusu athari za mazingira zinaosababishwa na taka za plastiki.

“Kufikia mwaka 2050 kama taka za plastiki zisipodhibitiwa, idadi ya taka za plastiki baharini, itazidi idadi ya samaki, kwa sababu  zaidi ya tani milioni nane za plastiki hutupwa baharini kila mwaka.

Ameongeza: “Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk John Magufuli imeanza kuchukua hatua za kupiga vita mifuko ya plastiki, ili kunusuru uhai wa viumbe vya baharini na nchi kavu.”

Dk Mduma alisema kupitia maudhui ya maadhimisho ya siku ya haki za mlaji kwa mwaka 2021, serikali wafanyabiashara na wadhibiti ubora na usimamizi wa mazingira wanashauriwa kuchukua hatua zitakazoshaimirisha kupiga vita taka za plastiki.

Amesema miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuongeza upelekaji wa elimu kuhusu haki na wajibu wa mlaji vinavyobainisha uhitaji wa kuishi katika mazingira bora na endelevu na wajibu wa kutunza mazingira.

“Serikali kupitia Wizara inayosimamia uhifadhi wa mazingira inaendelea na juhudi mbalimbali za kimkakati kuhakikisha kuwa inapunguza na hatimaye kutokomeza janga la bidhaa za plastiki katika mazingira yetu,” Amesema.

Nae Mfanyabiashara wa soko la Majengo Samson China ameiomba Serikali kudhibiti vifungashio hivyo kutoka viwandani ili visiingie sokoni hiyo itasaidia kwa wafanyabiashara kutafta njia nyingine ya kufunga bidhaa zao.

Amesema vipo viwanda vinavyojihusisha unauzalishaji wa vifungashio hivyo, hatua inatakiwa zianze kuchukuliwa kuanzia kwa wamiliki wa viwanda hivyo.

“Tunatambua tamko la Serikali la kuacha kutumia vifungashio vya plastiki lakinu tunaomba kabla ya kuja kutuchukulia hatua sisi wafanyabiashara wadogo kwanza waanze kufunga viwanda vya kuzalisha bidhaa hizo tunaamini hata mtaani vitapotea,” Amesema.

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Rukia Salumu, amesema ili kuondoa matumizi ya vifungashio vya plastiki Serikali inatakiwa kuongeza idadi ya uzalishaji wa vifungashio mbadala na kuweka bei ambayo kila Mwananchi anaweza kumudu.

Amesema wananchi wengi wanatumia vifungashio vya plastiki kwasababu havina gharama na hutolewa bure.

“Tunaiomba serikali ianze kudhibiti chanzo cha wananchi kutumia bidhaa za plastiki , baada ya hapo ianze kuchukua hatua kwa mwananchi mmoja mmoja atakaye kaidi sheria na taratibu zitakazowekwa,” Amesema Rukia Salum.

 

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani, Dk John Maduma akizungumza wakati wa kuhitimisha maadhimisho ya siku ya mlaji duniani.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2