Na Mwandishi Wetu, Chato
MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imesema, itaukumbuka mchango mkubwa wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati, Dkt John Pombe Magufuli kwa kumaliza changamoto ya maji Jijini Dar es salaam.
Hayo yamesemwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja, wakati akizungumza mchango wa Hayati Magufuli, katika Uwanja wa Magufuli, Chato ambapo mwili wa Hayati Magufuli, umeagwa leo.
"Dawasa tumeupokea msiba huu kwa mshituko mkubwa sababu Rais alikuwa na ziara ya mwisho kuja DAWASA katika siku tatu za ziara ya Dar es Salaam."
"Alikuwa anakuja kuzindua mradi mkubwa wa uboreshaji wa Maji kutoka Makongo hadi Bagamoyo uliogharimu takribani Bilion 67." amesema Mhandisi Luhemeja.
Ikumbukwe kuwa, Ilikua ni katika uzinduzi wa Upanuzi wa Mtambo wa Ruvu Juu Mkoa wa Pwani Juni 2017, akisisitiza na kuwataka DAWASA wafikishe huduma ya maji katika Mji wa Kisarawe moja ya miji ya kihistoria ndani ya Afrika Mashariki ambao hauna maji toka nchi ipate Uhuru.
DAWASA walitii agizo hilo kwa kutumia mapato ya ndani, mwaka 2019 aliyekuwa Makamu wa Rais kwa Kipindi hicho Samia Suluhu aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa Tanki la Ujazo wa Milioni 6 lililojengwa katika Mji wa Kisarawe, ujenzi wa Kituo cha kusukumia maji kutoka Tanki la Kibamba na ulazaji wa mabomba ya kusafirishia maji.
Mradi huo uliweza kuchukua mwaka mmoja kukamilika na mwaka 2020 iliandikwa historia toka nchini ipate uhuru mradi mkubwa wa maji wa Bilion 10.5 ukitekelezwa chini ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) baada ya kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt John Pombe Magufuli siku uliyokuwa unazindua upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu.
Mbali na mradi huo mkubwa wa Maji Kisarawe kukamilika uliweza kuzaa mradi mwingine wa Kisarawe -Pugu uliotekelezwa kwa thamani ya Bilion 5 ili kufikisha maji katika maeneo ya Pugu, Majohe, Chanika, Gongo la Mboto, Ukonga hadi Tabata Kinyerezi.
Aidha, wakati wa Uongozi wa Hayati Magufuli DAWASA wameweza kutekeleza mradi wa Mkuranga wenye thamani ya Bilion 5.6 uko mbioni kukamilika, ukitarajia kuhudumia wakazi 25,000 wa maeneo ya mji huo .
DAWASA imeweza kutekeleza miradi yote mikubwa na maboresho ndani ya Jiji la Dar es Salaam kwa kutumia fedha za ndani.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment