Na Amiri Kilagalila,Njombe
ZAIDI ya watumishi 50 kutoka mkoa wa Songwe wamefika mkoani Njombe ili kujifunza na kubeba ujuzi wa kufikia mafanikio ya usafi wa mazingira na ujenzi wa vyoo bora na vya kisasa inayopelekea halmashauri ya wilaya ya Njombe kufanya vizuri na kuongoza mfululizo kitaifa katika kampeni ya usafi wa mazingira.
Mkoa wa Songwe ni miongoni mwa mikoa ambayo bado ipo nyuma katika utekelezaji wa zoezi la usafi wa mazingira na ujenzi wa vyoo bora huku jamii ya mkoa huo ikiwa nyuma kwa kujenga vyoo visivyo na ubora,vingi vikitajwa kuwa katika kundi A na B.
Akizungumza baada ya semina ya siku ya kwanza iliyofanyika mjini Njombe,Katibu tawala wa mkoa wa Songwe Dkt,Seif Shekalage amesema wamefanikiwa kujifunza swala la ushirikiano kutoka ngazi ya chini katika jamii pamoja na kutoa elimu ya kutosha na kujitoa hatua iliyowafikisha katika mafanikio yao.
“Wenzetu wamefanikiwa jambo hili kwanza kwasababu ya ushirikiano mkubwa kuanzia ngazi ya chini kutoka kwa mwananchi,kutoa elimu kwa wananchi,kwa viongozi wa jadi,watu maarufu na walivyoelewa waliweza kutembea kwa pamoja.lakini la pili ni watu kujitoa ikiwemo kwa viongozi bila kujali kwamba lazima ulipwe”alisema Dkt,Seif Shekalage
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth Msafiri ambaye eneo lake limekuwa likiongoza mara kwa mara katika swala la usafi wa mazingira amesema hatua mbali mbali za ushirikishwaji wa kaya katika kampeni hiyo imewezesha wakazi wake kuwa na mapokeo chanya ya ujenzi wa vyoo bora na vya kisasa huku wakifanikiwa pia kuondokana na magonjwa ya mlipuko yaliyokuwa yakitokea awali kabla ya utekelezaji wa zoezi hilo.
Mkuu wa wilaya ya Songwe Samwel Opulukwa pamoja na timu ya wataalamu wa wilaya hiyo walioongozana na mkurugenzi,mara baada ya semina wametembelea katika kijiji cha Itunduma pamoja na Ibumila wamekiri kujifunza kikamilifu mafanikio ya vijiji hivyo kwenye kaya pamoja na taasisi za umma ndani ya wilaya ya Njombe huku wakiahidi kwenda kutekeleza katika wilaya yao ili kutekeleza zoezi la usafi kwa wananchi wa wilaya hiyo.
“Leo hii tumeona na kujifunza mengi hapa na mambo yote kwa asilimia 95 yamefanywa na wananchi wenyewe na viongozi,kwa hiyo wananchi wa hapa ni watanzania kama wananchi wa Songwe,tunaimani na sisi tutaweza”alisema Samwel Opulukwa
Awali mtendaji wa kijiji cha Itunduma Tabia Nkondola amesema kijiji hicho kimefanikiwa kwa 100% katika utekelezaji wa swala la usafi wa mazingira na ujenzi wa vyoo bora huku kaya zake zikiwa na vyoo vya daraja C na D pamoja na kutunukiwa cheti cha ubora daraja la pili.
Amesema licha ya mafanikio hayo lakini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ikiwemo kipato duni kwa baadhi ya kaya za wajane na wazee na kupelekea tatizo kumudu ghalama za ujenzi lakini wameendelea na mikakati mbali mbali ya kufanikisha kampeni hiyo ikiwemo kubadilishana uzoefu,ufuatiliaji,mikutano,elimu elekezi kwa wananchi na kutumia sheria ndogo ndogo.
“Mikakati ya hapo badaye ni kuendelea kuhamasisha wananchi wenye kaya zenye vyoo vya C kujenga vyoo vya daraja D na matarajio yetu hadi kufikia April 2022 vyoo vyote vitakuwa vyenye daraja D na kwa wale wanaojenga kaya mpya watalazimika kujenga vyoo vya daraja C”alisema Tabia Nkondola
Zawadi Nyagawa,Hassan Mgoba na Chales Mlonganile ni baadhi ya wakazi wa vijiji vya Itunduma na Ibumila wamesema elimu iliyokuwa ikitolewa na viongozi wao pamoja faini ndogo ndogo zimewawezesha kuwa na kaya zenye vyoo bora huku wakiepukana na maradhi.
Timu ya wataalamu iliyoongozana na mkuu wa wilaya ya Songwe wakiwa nje ya ofisi ya kata ya Itunduma wilayani Njombe na kupiga picha katika kibao cha kampeni ya usafi wa mazingira walipotembelea katika vijiji hivyo kujifunza namna vilivyofanikiwa katika kampeni.
Wataalamu kutoka Songwe wakijifunza eneo la kunawa mikono kwa watoto wa shule ya msingi Ibumila baada ya kutoka chooni.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment