Charles James, Michuzi TV
MPUUZENI! Ni kauli iliyotolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Utumishi ambaye amewataka watanzania kupuuza kauli iliyotolewa na aliyekua Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof Mussa Assad aliyesema watumishi wa umma hawana uwezo.
Hivi karibuni akiwa kwenye mdahalo ulioandaliwa na Chuo cha Kiislamu mkoani Morogoro, Prof Assad alisema asilimia 60 ya watumishi wa umma hawana uwezo huku asilimia 40 wakiwa na uwezo mdogo huku akishauri wale wasio na uwezo wapigwe chini.
Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma, Katibu Mkuu Utumishi, Dk Laurean Ndumbaro amewataka watanzania kumpuuza Prof Assad akisema kauli hiyo haina ukweli wowote na badala yake imejaa ukakasi huku ikiwa imetolewa kwa kuongozwa na hisia.
Dk Ndumbaro amesema yeye akiwa kama mtu anayesimamia wizara inayohusika na utumishi anawahakikishia kwamba watumishi wote wa umma wapo katika ofisi zao kwa sababu wamekidhi viwango na sifa zote zinazohitajika na hivyo kuwataka watanzania kuacha kusikiliza matamko yanayotolewa kwa mihemko.
" Ni wito wangu kwa watanzania kupuuza matamko yanayotolewa kwa mihemko, jamii inapaswa kutambua kuwa utumishi wa umma unajengwa na kuongozwa na misingi ya katiba, sheria na taratibu ambapo nyaraka hizo ndizo zinazoongoza na kuelezea vigezo na sifa za ajira na ngazi za vyeo vya uongozi.
Mtu anapojitokeza na kusema kwamba asilimia 60 ya watumishi hawafai na 40 wana uwezo mdogo na yeye alikua mtumishi wa umma sasa tumueke kundi gani?
Ni wazi Prof Assad alisukumwa zaidi na hisia katika kuwasilisha hoja zake badala ya uwezo wake alionao, yeye ni Profesa alitumia tafiti kuzungumzia takwimu hizo? Nimsihi kutumia taaluma yake katika kuchanganua mambo na siyo mihemko na hisia," Amesema Dk Ndumbaro.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment