DOTTO JAMES AKABIDHIWA RASMI OFISI, AAHIDI KUSHIRIKIANA NA WATUMISHI WOTE KUKUZA SEKTA YA VIWANDA NA BIASHARA NCHINI | Tarimo Blog






KATIBU Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dotto James amekabidhiwa ofisi rasmi na  aliyekuwa Katibu Mkuu  wa Wizara hiyo, Prof Riziki Shemdoe aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI  leo katika ofisi za Wizara ya Viwanda na Biashara  zilizopo Mtumba jijini  Dodoma.

Makatibu Wakuu hao waliahidi kuendelea kushirikiana katika kazi mbalimbali hasa katika kuboresha muundo wa Maafisa Biashara wa Halmashauri kwa kuanzisha Kitengo cha Viwanda, Biashara na Uwekezaji ili kurahisisha utendaji kazi  wa wizara hizo kukuza biashara na kuendeleza viwanda  vikubwa na vidogo vidogo vilivyopo katika halmashauri hizo.

Akizungumza wakati akiwashukuru wafanyakazi wote wa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kufanya naye kazi vizuri kwa ushirikiano na Amani, Katibu Mkuu TAMISEMI  ametoa angalizo  kwa Wizara  kuendelea  kusimamia  upatikanaji wa Sukari, Mafuta ya Kula, Mfumuko wa bei wa vyakula hasa katika mfungo wa mwezi ramadhani,  na  masoko kwa ajili ya mazao ndani na nje ya nchi.

Kwa upande Katibu Mkuu Dotto amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua na kumuamini katika nafasi hiyo kwenye wizara nyeti inayochochea ukuaji wa uchumi wa Nchi na kuahidi kuifanya kazi hiyo kwa weledi mkubwa akishirikiana na watendaji na watumishi katika kunyanyua sekta ya Viwanda na Biashara.

" Wote tunafahamu kwamba ukuaji wa Viwanda na Biashara ni chachu kubwa pia ya kukuza uchumi wa Taifa letu, na sisi ndio wizara yenye dhamana ya kusimamia ukuaji huo, niwaombe wote tufanye kazi kwa uadilifu na wivu mkubwa kwa nchi yetu huku tukishirikiana kwa pamoja, lengo ni kumsaidia kazi Rais wetu Mama Samia katika kuwatumikia watanzania," Amesema Katibu Mkuu Dotto James.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2