SERIKALI imesema katika nyakati hizi za mabadiliko makubwa ya kitaaluma na teknolojia duniani itaendelea kuwekeza na kuwaandaa wataalamu wake ili waweze kushindana katika soko la kimataifa.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamadi Masauni wakati akizindua na kushuhudia utiaji saini wa makubaliano ya kushirikiana baina ya Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA) na Taasisi ya Kimataifa ya Uhasibu yenye makao makuu yake Uingereza (ACCA).
Makubaliano ya pande hizo mbili yamelenga kuinua tasnia ya Uhasibu nchini kwa kuhakikisha kwamba wahasibu wengi wa Tanzania wale waliopo makazini na mashuleni wanapata mafunzo haya ambayo yatawakuza kuweza kuwa wahasibu wanaotambulika kimataifa.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Naibu Waziri Masauni amesema kuanza kufundishwa kwa masomo hayo nchini kutaipunguzia gharama serikali ya kupeleka wahasibu wake nje ya nchi kusoma hivyo kitendo cha kusoma hapa hapa nchini kitaokoa kiasi kikubwa cha fedha kilichokua kikipelekwa nje ya Nchi.
" Ni furaha sana kuona sasa tutazalisha wenyewe wataalamu wetu wa uhasibu katika kiwango cha kimataifa, licha ya kwamba tutaondoa gharama ya serikali kuwasomesha watu wake nje kwenye kada hii lakini sasa tutapata faida kwa kuwa sisi pia tutaanza kupokea wanafunzi kutoka Nchi jirani.
Katika Dunia ya sasa iliyotawaliwa na wasomi kama Taifa inabidi tutengeneze watu wetu wenyewe wanaoweza kushindana katika soko la kimataifa, niwatake Mhasibu Mkuu wa Serikali na Mkaguzi wa Ndani wa Serikali kuhakikisha mnasimamia na kuinua watalaamu wetu katika kada ya Uhasibu," Amesema Naibu Waziri Masauni.
Amekipongeza Chuo cha IAA na Taasisi ya ACCA kwa kuanzisha masomo hayo nchini ambayo anaamini yanaenda kuwa na manufaa na watanzania na yenye tija kwa Taifa pia.
Kwa upande wake mratibu wa mafunzo hayo kutoka IAA ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Uhasibu ya Chuo hicho ameishukuru serikali kupitia wizara ya Fedha kwa kuwaunga mkono na kuwafanya kuwa Chuo cha kwanza nchini kuanzisha masomo hayo lakini pia kikiwa mojawapo ya vyuo vitatu pekee vinavyotoa mafunzo hayo katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Amesema mafunzo hayo ya Uhasibu kimataifa yataendeshwa katika Mikoa mitatu ya Arusha, Dar es Salaam na Dodoma na yamezingatia mahitaji ya wanafunzi wasioweza kusafiri ambapo watawasiliana nao kuweza kutoa mafunzo hayo ya ndani.
Nae Mwakilishi wa Taasisi ya ACCA, Jenard Lazaro ameikipongeza Chuo cha IAA kwa kuanzisha masomo hayo ambayo yatakua na tija kwa Taifa huku pia akiishukuru Serikali kwa namna ambavyo imekua ikishirikiana nao kwa muda mrefu.
Amesema mpaka sasa Tanzania kuna idadi ya wanachama wa ACCA wapatao 400 nchi nzima na kuanzishwa kwa masomo hayo hapa nchini kutachochea zaidi wingi wa wataalamu wa Uhasibu kimataifa.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment