Charles James, Michuzi TV
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka watumishi wa wizara yake kuepukana na vitendo vinavyoharibu taswira ya utumishi wa umma vikiwemo vitendo vya rushwa na ubabe.
Hayo ameyasema leo jijini Dodoma wakati akifungua Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo sekta ya Mifugo ambapo amesisitiza nidhamu, heshima na uwajibikaji kwa watumishi wote.
Waziri Mashimba amewataka watumishi wa sekta ya Mifugo kuzingatia uadilifu na uwajibikaji katika utekelezaji wa shughuli za serikali huku akisema siyo vema kwa mtumishi wa umma kukutwa katika skendo na matukio maovu yanayoharibu taswira ya serikali.
" Niwaase watumishi wote kuepuka vitendo vinavyoenda kinyume na Sheria za Nchi yetu na taratibu za kazi, haileti picha nzuri kuona mtumishi wa umma anatajwa kwenye kashfa za rushwa hili siyo jambo jema hata kidogo, epukeni rushwa.
Ubabe mahali pa kazi pia haufai nitoe rai kwenu kuzingatia nidhamu na heshima ili tuweze kufanya kazi kama Timu na kufanikiwa ni lazima tupendane, tuheshimiane bila hivyo ni vigumu kufanikiwa pamoja.
Mtumie Baraza hili kujadili bajeti iliyopita na bajeti yetu ya mwaka huu, nyinyi nyote mnapaswa kuwa wasimamizi na watekelezaji wa bajeti ya wizara na hasa sekta yenu ya mifugo, siyo suala la kumuachia Waziri, Naibu Waziri au Katibu Mkuu ni letu sote tushirikiane katika kutekeleza bajeti yetu," Amesema Waziri Mashimba.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara hiyo, Prof Elisante Ole Gabriel amemuahidi Waziri Mashimba kuendelea kusimamia kwa nguvu sekta ya Mifugo pamoja na kuyafuata maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alisema hatopenda kuona Mifugo imekonda.
" Tukuahidi Mhe Waziri kwamba kupitia Baraza hili tunaenda pia kuangalia suala la bajeti yetu, kuangalia namna ya kuboresha sekta yetu ya Mifugo ili tuweze kuwanyanyua wafugaji wetu kutoka kufanya ufugaji wa mazoea na kwenda kufanya ufugaji wa biashara ambao utakua na tija kwao na kwa Taifa kwa ujumla, " Amesema Prof Ole Gabriel.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment