MBUNGE HHAYUMA AWATAKA WANAFUNZI NANGWA WAFAULU ILI NA KUMUENZI RAIS SAMIA NA HAYATI DKT MAGUFULI | Tarimo Blog

Na Mwandishi wetu, Hanang'

MBUNGE wa Jimbo la Hanang' mhe Samwel Hhayuma Xaday amewasihi wanafunzi wasichana wa kidato cha sita wa shule ya Sekondari Nangwa, wanaotarajia kufanya mtihani wa kidato cha sita Mei 3 mwaka huu, kufaulu mitihani hiyo ili kumuenzi hayati John Magufuli ambaye ameachia alama kwenye nidhamu ya kufanya kazi kwa kufanikisha miradi ya kimkakati na pia kumuenzi Rais wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan ambaye ni mwanamke wa kwanza kuwa Rais hapa Tanzania.

Hhayuma ameyasema hayo kwenye mahafali ya 15 ya shule ya Sekondari ya Nangwa ambapo amesema hayati Dkt Magufuli aliacha kauli mbiu ya hapa kazi tuu na Rais Samia ambaye watanzania wana matumaini makubwa kwake kupitia kauli mbiu yake ya kazi iendelee.

Amesema wasichana hao wamepata elimu ya kidato cha sita hivyo ili kuwaenzi viongozi hao wafaulu mitihani yao kwani wameelimika na anatarajia watapata alama 100 kwa kila somo.

"Mnapaswa kuonyesha faida ya kuelimika, elimu iwatofautishe na wengine ambao hawajaipata, unapaswa hata ukilima shamba ulime kitaalam upate mazao yenye tija, utajiri mwingi upo shambani na kwenye mifugo, haitakuwa na maana utoke shule siku ya mwisho kisha uwe kama ulivyoingia siku ya kwanza" amesema.

Ameahidi kumaliza changamoto ya vitabu kwa shule zote tatu za kidato cha sita zilizopo kwenye wilaya hiyo na kufanikisha bonanza la michezo la wilaya hiyo litakalofanyika hivi karibuni ikishirikisha michezo ya riadha, soka na mpira wa pete.

"Pamoja na hayo nitaipigania barabara ya Nangwa, Simbay, Gisambalang inayokwenda hadi Kondoa kuwa ya lami ili wana Hanang' wapate fursa ya kusafirisha kwa urahisi kwenda Dodoma, mazao yao ya mbaazi, ngano, mahindi na chumvi pamoja na saruji," amesema.

Mkuu wa shule ya sekondari Nangwa, mwalimu Esta Malongo amesema wanafunzi huwa wanajitahidi kufanya vizuri kitaaluma kwani kwenye mitihani ya Taifa kila mwaka wanafaulu kwa daraja la kwanza, pili na tatu pekee.

Mwalimu Malongo amesema shule hiyo ina watumishi 36 kati yao walimu ni 20 na watumishi 15 wakiwemo 13 wa ajira ya muda mfupi na wawili wa ajira ya kudumu.Hata hivyo, ameiomba Serikali kuwajengea uzio ili kuwaepusha wanyama wanaoingia usiku shuleni hapo wakiwemo fisi wanaowapa kero wanafunzi wanaojisomea.

Mmoja kati ya wanafunzi hao, Latifa Shabani amesema shule yao ina tahasusi sita na wanafunzi 509 wakiwemo wa kidato cha sita 245 na kidato cha tano 264.

Latifa amesema picha halisi ya watahiniwa wa mwaka huu 2021 inaonyesha dhahiri kuwa watafaulu kwa asilimia 100 kutokana na picha ya matokeo ya ndani na ya ujirani mwema.

 

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2