· Alikuwa Balozi na mtetezi wa Kiswahili
· Watanzania tumuenzi kwa kukiendeleza
(Na Jovina Bujulu)
Hivi karibuni Taifa la Tanzania limepata pigo la kuondokewa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ambaye atakumbukwa kwa mambo mengi aliyoyafanya katika kuliendeleza na kulifanya kuwa miongoni mwa mataifa yanayokua kwa kasi katika nyanja mbalimbali.
Lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa mambo ambayo Hayati Dkt. Magufuli aliyasimamia kwa nguvu zake zote katika kuiendeleza na kuikuza ambapo kwa sasa Kiswahili ni miongoni mwa lugha zinazoheshimika na kutambuliwa ulimwenguni ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya watumiaji wake kutoka katika nchi mbalimbali.
Hayati Dkt. Magufuli hakusita kuonyesha wazi wazi utashi wake wa kuikuza lugha hii hasa wakati wa mikutano mbalimbali ya ndani ya nchi na hata katika mikutano aliyoifanya na viongozi wa mataifa ya nje ambapo alidiriki kuongea kwa kutumia lugha ya Kiswahili na hata kuwafanya viongozi wa mataifa ya nje katika mikutano yake kuongea maneno machache ya Kiswahili na wengine kutoa hotuba zao kwa lugha ya Kiswahili.
Ni Hayati Dkt. Magufuli ambaye aliweza kuwashawishi viongozi wa mkutano wa 39 wa Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kukubali Kiswahili kutumika katika mawasiliano ya Jumuiya hii ambapo Wakuu hao walilipitisha wazo hilo bila kupingwa na sasa lugha ya Kiswahili inatumika katika mawasiliano ya SADC. !
Aidha mapenzi yake kwa lugha ya Kiswahili hakuweza kuyaficha hasa pale alipofanya ziara katika nchi mbalimbali hasa za Kusini mwa Afrika ambapo alidiriki kuwapatia vitabu vya Kiswahili baadhi ya marais. Alitoa vitabu kwa Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ili aweze kujifunza Kiswahili ambapo naye kwa kuonesha kulikubali wazo la Hayati Magufuli alisema nchi yake itaanza kutumia lugha ya Kiswahili kufundisha katika shule za msingi na sekondari ambapo hivi karibuni katika msiba wa hayati Magufuli alisema kwamba hilo limekwisha tekelezwa na somo la Kiswahili sasa linafundishwa kama somo shuleni nchini Afrika Kusini.
Rais Ramaphosa alisema, “ Napenda kumshukuru Rais Magufuli kwa kuwa mwana Umajumui au mwana Afrika ambaye aliona kwamba Uafrika, mila na desturi zapaswa kuheshimiwa ikiwa ni pamoja na kukumbatia na kuzingatia lugha zetu, alikuwa mwinjilisti, alitaka kila mwafrika barani Afrika aweze kuzungumza Kiswahili, na aliponitembelea Afrika Kusini alinipatia boksi la vitabu nami nilimweleza kuwa nitampatia zawadi na zawadi tuliyompatia ni kuifanya lugha ya Kiswahili kufundishwa shuleni na sasa Kiswahili kinafundishwa shuleni Afrika Kusini”
Aidha, katika msiba huo, Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi alihutubia kwa lugha ya Kiswahili huku akimnukuu Hayati Dkt. Magufuli kuwa alisema “ Kiswahili ni lugha ya SADC, kwa hiyo naomba mnisamehe kwa makosa kwa shauri leo itabidi nisema Kiswahili”. Utashi wa Hayati Dkt. Magufuli kwa lugha ya Kiswahili ulimfanya Rais Nyusi kumuenzi kwa kuhutubia kwa lugha ambayo aliwaambia kuwa ni lugha ya SADC.
Katika kusisitiza utashi wake wa dhati kuhusu kueneza lugha ya Kiswahili, Hayati Dkt. Magufuli pia aliwahi kuwapatia zawadi ya vitabu vya Kiswahili Wakuu wan chi wote wa SADC wakati wa Mkutano wao wa 39 ambao ulifanyika jijini Dar es salaam ili waende navyo nchini mwao kwa ajili ya kujifunza lugha hiyo.
Hakika hakuna ubishi kuwa katika kipindi cha uongozi wake lugha ya Kiswahili imepiga hatua kubwa kutokana na viongozi na wasaidizi wake waliokuwa wakimwakilisha nje ya Tanzania kuwa na ujasiri wa kuzungumza lugha hii katika majukwaa ya Kimataifa. Hayati Dkt. Magufuli alikuwa ni kiongozi aliyesimamia kwa vitendo kukuza Kiswahili ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Katika hotuba yake ya kukabidhi Uenyekiti wa SADC kwenye mkutano wa 40 Hayati Dkt. Magufuli alisema, “ Ni imani yangu kuwa kuridhiwa kwa lugha hii ya kwanza ya Kiafrika kwenye Jumuiya yetu, kutachochea ushirikiano na utengamano ndani ya Jumuiya, na hii ndiyo sababu nimeamua kutoa hotuba yangu kwa Kiswahili na nimefarijika kuwaona kuwa, wengi wenu mnanisikiliza bila kutumia vifaa vya kutafsiri. Hii inaonesha kuwa mnaifahamu na kuielewa vyema lugha ya hii adhimu ya Kiswahili”.
Aidha, Hayati Dkt. Magufuli alisisitiza lugha ya Kiswahili kutumika katika mikutano ya kisheria, maandishi ya kisheria na mahakamani ambapo kwa kuonesha dhamira ya kweli katika kutumia Kiswahili kwenye taasisi za umma aliweza kumpandisha cheo Jaji Zepharine Nyalugenda Galeba kutoka kuwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma na kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani kutokana na kutoa hukumu kwa lugha ya Kiswahili.
Mchango wa Hayati Dkt. Magufuli katika maendeleo ya Kiswahili ni makubwa sana kwani mbali na kuitambulisha lugha hii Kimataifa, ameweza kukuza fasihi ya Kiswahili, kukuza msamiati, kuongeza fursa za ajira kwa wataalamu wa Kiswahili, kuwatia ari wakalimani na wafasiri na kuwahimiza wananchi kuthamini matumizi ya lugha ya Kiswahili.
Msukumo uliooneshwa na hayati Dkt. Magufuli katika kuikuza, kuiendeleza na kuineza lugha ya Kiswahili kumeifanya lugha hii kukubaliwa hivi karibuni kuwa moja ya lugha za mawasiliano zitakazotumika katika Umoja wa Nchi Zinazozalisha Madini ya Almasi Afrika (ADPA).
Katika kuhakikisha kuwa Tanzania inaenzi mchango mkubwa uliotolewa na Hayati Dkt. Magufuli katika kuitangaza lugha ya Kiswahili, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa alipokuwa akiwasilisha Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa 2021/22, alisisitiza kwamba Serikali itatekeleza mambo muhimu ikiwemo kuenzi lugha ya Kiswahili.
Hakika, Hayati Dkt. Magufuli atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika ukuzaji na uenezaji wa lugha ya Kiswahili, kwani aliweza kukivusha nje ya mipaka ya Tanzania, ukanda wa Afrika Mashariki na Dunia nzima kwa ujumla. Pumzika kwa Amani mtetezi wa Kiswahili.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment