MRADI WA MAJI LIKUYU WAFIKIA ASILIMIA 90,KAMATI YA SIASA YAPONGEZA UTEKELEZAJI WAKE | Tarimo Blog

Na Muhidin Amri,Namtumbo

KAMATI ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi(CCM)Mkoa wa Ruvuma imetembelea mradi mkubwa wa maji katika kijiji cha Likuyuseka wilaya ya Namtumbo unaotekelezwa na wakala wa maji vijijini (Ruwasa). 

Mradi huo unaogharimu shilingi bilioni 3,578,363.191 utawezesha wananchi wapatao 13,319 wa kijiji cha Likuyuseka na Mandela kupata maji safi na salama. 

Akiongea baada ya kutembelea mradi huo,Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoani Ruvuma Oddo Mwisho, ameipongeza wizara ya maji kupitia wakala wa maji vijijini (Ruwasa) kutekeleza mradi huo ambao unakwenda kutatua kero ya maji kwa wananchi wa vijiji hivyo. Aidha alisema, utaratibu wa kujenga miradi ya maji kwa njia ya Force Akaunti unaotumiwa na Ruwasa kujenga miradi ya maji katika maeneo mbalimbali umesaidia kuokoa fedha nyingi na kuharakisha ujenzi wa miradi ya maji. 

Amempongeza meneja wa Ruwasa wilaya ya Namtumbo David Mkondya na meneja wa Ruwasa mkoa Rebman Ganshonga kwa kusimamia vyema ujenzi wa mradi huo na miradi mingine ya maji inayojengwa na kuwataka wananchi kushirikiana na serikali kutunza na kulinda miundombinu ya maji.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ameitaka kamati ya maji kuhakikisha fedha zinazopatikana kutokana na mauzo ya maji zinapelekwa benki, badala ya kuweka ndani ili kuepusha kutumika vibaya. 

Mndeme ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa amewataka wajumbe wa kamati ya maji kuwa wazalendo na kusisitiza kuwa,mradi utakapoanza kazi atapeleka mkaguzi ili kuangalia mapato na matumizi ya fedha kama zinatumika vizuri. 

Alisema, mradi wa maji Likuyuseka ni mkubwa na umegharimu fedha nyingi za walipa kodi wa nchi hii,kwa hiyo ni lazima jumuiya ya watumia maji kwa niaba ya wananchi kushirikiana na serikali ya kijiji kusimamia vyema uendeshaji wa mradi huo pamoja na fedha zitakazo patikana.
Mndeme,ameipongeza Ruwasa kwa kusimamia kikamilifu mradi huo kuanzia hatua ya awali hadi sasa, na utakapo kamilika utawezesha wananchi wa kijiji cha Likuyuseka na Mandela kupata maji safi na salama. 

Kwa upande wake meneja wa Ruwasa wilaya ya Namtumbo David Mkondya alisema, mradi huo umekamilika kwa asilimia 90 na unatekelezwa chini ya program ya maendeleo ya Sekta ya maji(WSDP) kupitia program ndogo ya maji na usafi wa mazingira vijijini(RWSSP). Alisema, mkataba wa ujenzi ulisainiwa mwezi Oktoba 2017 na utekelezaji rasmi wa ujenzi ulianza mwezi Novemba 2017 na ulitarajiwa kukamilika mwezi Januari 2020 chini ya mkandarasi Kampuni ya Elegance Developers Co Ltd kwa gharama ya shilingi bilioni 4,915,864,910.00. 

Hata hivyo alieleza kuwa,serikali kupitia wizara ya maji ilivunja mkataba na mkandarasi na kukabidhi mradi huo kwa Ruwasa kwa ajili ya kukamilisha kazi zilizobaki. Kwa mujibu wa Mkondya, baada ya Ruwasa kukabidhiwa mradi na kuendelea na kazi, gharama za ujenzi zimepungua kutoka bilioni 4,915,864,910.00 hadi kufikia bilioni 3,578,363,191 na hatua hiyo imetokana na Ruwasa kujenga mradi huo kwa njia ya force Akaunti. 

Alisema, gharama hizo zimetokana na kazi zilizofanywa na mkandarasi kulipwa pamoja na gharama za kukamilisha mradi huo na hadi sasa fedha zilizotumika ni shilingi bilioni 3,070,057,843 na mradi umefikia asilimia 90. 


 

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2