Njombe:Takukuru yazidi kuwang'ata waliotafuna fedha za vyama vya ushirika | Tarimo Blog

Na Amiri Kilagalila,Njombe

Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) mkoani Njombe imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi milioni 29,802,646 kutoka kwa wadaiwa sugu waliokopa katika vyama vya ushirika vya AMCOS, SACCOS pamoja na benki ya Njocoba.

Hayo yamesemwa leo na mkuu wa Takukuru mkoa wa Njombe Kassim Ephrem wakati alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa oparesheni ya taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu iliyofanyika hapa mkoani Njombe.

Amesema katika vyama vya AMCOS na SACCOS shilingi milioni 23,003, 000 zimeokolewa kutoka kwa wadaiwa hao huku kiasi cha milioni 6,799,646 kikikusanywa kutoka wadaiwa wa benki ya Njocoba.

Amesema taasisi hiyo pia imesaidia kukusanya jumla ya shilingi milioni 22,462,886.26 ambazo zimeokolewa kutoka kwa wadaiwa sugu wa mfuko wa taifa wa hifadhi jamii (NSSF) tangu walipoanza zoezi la kuwafuatilia waajiri ambao hawawasilishi michango ya wanachama wa mifuko hiyo.

Amesema katika zoezi hilo Takukuru pia imefanikiwa kukusanya na kuokoa shilingi milioni 31,635,000 kutoka kwa wadaiwa sugu wa mfuko wa pembejeo za kilimo (AITF) ambao ni wadaiwa mmoja mmoja.

"Napenda kutumia fursa hii kuwahimiza waajiri wote kuhakikisha kuwa wanawasilisha kwa wakati makato ya michango ya watumishi wao kwa mifuko ya hifadhi ya jamii bila shuruti" amesema Kassim.

Amesema katika kuchunguza makosa ya rushwa kama sehemu ya majukumu ya taasisi hiyo wameweza kuokoa kiasi cha shilingi milioni 67,931,432 ambazo kama wasingeingilia kati zingeishia katika mikono ya wahalifu na kushindwa kufanya kazi iliyokusudiwa.

Amesema kuwa  fedha hizo zimeokolewa kutokana na taarifa mbalimbali ambazo walizipokea zikihusisha tuhuma za rushwa na ubadhilifu.

Amesema pamoja na kuokoa fedha hizo taasisi hiyo imeendesha jumla ya kesi 10 katika mahakama za wilaya ya Njombe na Makete zilizotokana na makosa mbalimbali yakiwemo ya rushwa na yasiyo ya rushwa.

Amesema katika kipindi hicho kesi nne zilizokuwa zikiendeshwa katika mahakama ya wilaya ya Makete zimetolewa hukumu na watuhumiwa katika kesi hizo zote walitiwa hatiani.

"Washtakiwa watatu walihukumiwa kila mmoja kifungo cha miaka mitatu jela na kutakiwa kurejesha fedha walizofanyia ubadhilifu kwenye halmashauri ya wilaya Makete pindi wamalizapo vifungo vyao" amesema Kassim.

 

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2