MTEJA AIBURUZA VODACOM MAHAKAMANI | Tarimo Blog

MTEJA wa Kampuni ya Vodacom Francis Mosha amefungua kesi ya madai dhidi ya Kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania akidai fidia ya shilingi Milioni 26 kwa kumkata kiasi cha shilingi 2936 kwenye akaunti yake ya M-Pesa.

Madai hayo namba 57 ya mwaka 2021 yapo katika Mahakama ya wilaya ya Kinondoni mbele ya hakimu Mkazi Happy Kikoga ambapo leo Aprili 15, 2021 yaliitwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.

Katika madai yake, Mosha kupitia wakili wake Michael Merere anadai kwambaJanuari 8, 2020 bila sababu za msingi kupitia akaunti yake ya M-pesa kiasi cha sh. 20,000 kilikatwa na kwamba tatizo hilo lilijirudia Januari 9, 2021 ambapo kiasi cha shilingi 9136 kilikatwa kutoka katika akaunti yake ya M-Pesa.

Amedai baada ya Matukio hayo mawili mlalamikaji aliwasiliana na muhudumu wa Vodacom ambaye alimweleza tatizo hilo litafanyiwa kazi, lakini miezi mitatu ilipita na hakuna hatua yeyote iliyochukuliwa na Vodacom.

Kufuatia hali hiyo ya uzembe wa Vodacom au kushindwa kutilia maanani madai yake mdai, aliamua kuajiri Mwanasheria ambaye alipeleka madai kwa walalamikiwa, pamoja na kupolekewa barua hiyo, majibu ya Vodacom yalikuwa si ya kurudhisha kwa kuzingatia kuwa pesa za Mdai hazikurudishwa kwa takribani miezi minne, kitendo hicho kilimsababishia hasara hiyo.

Kufuatia hasara hiyo Mosha anaiomba Mahakama waiamuru Vodacom imlipe fedha hizo kiasi cha shilingi 26496320.

Hata hivyo katika majibu ya Vodacom Tanzania kupitia wakili wake Elizabeth Chacha wamekanusha madai hayo na kuwasilisha pingamizi la awali wakiiomba Mahakama itupilie mbali ombi hilo kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Pia wamedai kuwa madai hayo si ya kweli na kwamba hakuna hasara yeyote ambayo Mdai ameipata kwa sababu hela hizo zilikatwa kimakosa na zilisharudishwa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 21, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa ili kuipangia tarehe ya kuanza kusikilizwa kwa pingamizi hilo kabla ya kesi ya msingi.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2