WAKAZI wa kijiji Kipapa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, wameishukuru wizara ya maji kupitia wakala wa usambazaji maji safi na usafi wa mazingira vijijini (Ruwasa) kufikisha huduma ya maji safi na salama.
Wakizungumza jana mbele ya naibu waziri wa maji Maryprisca Mahundi wamesema, awali walipata shida kubwa ya kukosa maji safi,hali iliyosababisha kuhatarisha afya zao kwa kutumia maji kutoka kwenye vyanzo ambavyo sio salama.
Basilius Komba alisema, watahakikisha wanatunza miradi na miundombinu yote ya maji na kuwachukulia hatua watu wanaofanya shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo na kuchungia mifugo kwenye vyanzo ya maji.
Pensia Kowelo alisema,awali walilazimika kwenda mbali kufuata maji kwa matumizi yao ya kila siku jambo lililorudisha nyuma maendeleo yao kwa kuwa walipoteza muda mwingi kwenda kutafuta maji badala ya kushiriki katika kazi za maendeleo.
Mbunge wa jimbo la Mbinga vijijini Benaya Kapinga, ameipongeza wizara ya maji kukamilisha ujenzi wa miradi ya maji ambayo imemaliza kero ya wananchi wa jimbo hilo kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji.
Hata hivyo,ameiomba Serikali kuhakikisha inatoa fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji katika jimbo hilo ili ziweze kukamilisha miradi iliyoanza kujengwa na wananchi wafaidi matunda ya serikali yao.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa maji Maryprisca Mahundi amewataka wananchi kuacha kufanya shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji ili kulinda vyanzo hivyo na miundombinu ya maji inayojengwa kwa gharama kubwa.
Alisema, serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji na kuwapongeza wananchi wa kijiji hicho kwa kuendelea kushirikiana na serikali kwenye ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema, wizara ya maji imedhamiria kutekeleza na kukamilisha miradi yote ya maji ili kumaliza kero kwa wananchi ambao wanalazimika kutumia muda mwingi kwenda kutafuta maji kwa matumizi yao ya kila siku.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri,serikali tangu ilipoanzisha wakala wa maji vijijini Ruwasa imepunguza kwa asilimia kubwa kero ya upatikanaji wa huduma ya maji hapa nchini na kuwataka wananchi kuwa na imani na serikali yao.
Ametoa wiki moja kwa meneja wa wakala wa maji vijijini Ruwasa wilaya ya Mbinga na meneja wa Ruwasa mkoa wa Ruvuma kuhakikisha wana maliza tatizo la kutojaa maji haraka kwenye moja ya tenki linalotumika kusambaza maji kwa wananchi wa kijiji hicho.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment