SERIKALI imewataka watumishi wake nchini kuwa mfano wa kuigwa mbele ya jamii kwa kuwa wenye maadili huku wakizingatia nidhamu kwenye maeneo yao ya kazi na kwenye jamii inayowazunguka.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi wakati akizungumza kwenye kikao kazi cha Wizara hiyo kilichoendeshwa na Waziri wa wizara hiyo, Mohammed Mchengerwa jijini Dodoma.
Ndejembi amesema ni jambo la ajabu kuona mtumishi wa serikali anakua wa kwanza kufanya vitendo ambavyo siyo vya kimaadili kazini au kwenye maeneo ya nje ya kazi jambo ambalo linaitia doa serikali na hivyo kusisitiza utii na nidhamu kwa watumishi hao.
Ndejembi amesema kumekuepo na tabia ya watumishi kutokua na lugha za staha kwa wananchi wanaofika kupata huduma kwenye ofisi za serikali ambapo amekemea tabia hiyo akisisitiza kwamba watachukulia hatua wote wanaoenda kinyume na maadili ya kazi.
" Zipo taarifa za watumishi wanaotoa lugha mbaya kwa wananchi wanaofika kupata huduma, wengine lugha za ubabe na wakichelewesha huduma kwa mteja, niseme tu hatutomvumilia mtumishi wa namna hii kwa sababu atakua anaigombanisha serikali na wananchi.
Siyo kwenye maeneo ya kazi tu hata kwenye makazi yetu tunapaswa kuwa mfano mzuri wa watu wenye maadili, siyo mtumishi wa serikali ndio unaongoza kwa kupiga mkeo kila siku, mtumishi wa serikali unaongoza kwa ulevi na lugha chafu au unaongoza kwa madeni, tuziepuke sifa hizo mbali ili kulinda sura ya Serikali yetu," Amesema Ndejembi.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment