WAZIRI MCHENGERWA AWAPA NENO MA-RC NA MA-DC WANAOTUMIA MAMLAKA YAO KUWEKA WATU NDANI | Tarimo Blog





Charles James, Michuzi TV

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Mohammed Mchengerwa amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuacha kutumia vibaya mamlaka zao kuwaweka ndani kinyume na sheria watu wanaotenda makosa huku akiwataka kuzingatia Utawala wa haki na sheria.

Hayo ameyasema jijini Dodoma wakati akizungumza na watumishi wa Wizara yake ikiwa ni siku kadhaa tangu ateuliwe na Rais Suluhu Hassan kushika nafasi hiyo akichukua nafasi ya Kepteni George Mkuchika ambaye ameteuliwa kuwa Waziri asiye na wizara.

Akizungumza katika kikao hiko, Mchengerwa amesema Wakuu wengi wa Mikoa na Wilaya wamekua wakitumia vibaya mamlaka yao waliyopewa kikatiba ya kuwaweka ndani masaa 24 hadi 48 watu waliofanya makosa huku akisisitiza viongozi hao kutambua kuwa Serikali ya Rais Samia inazingatia haki na utawala bora.

Waziri Mchengerwa pia ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kuondoa kesi zote zilizopo mahakamani ambazo wanaona kwamba serikali haina uelekeo wa kushinda.

" Kumekua na mfulululizo wa kesi nyingi ambazo TAKUKURU inazipeleka mahakamani lakini haina ushahidi wa kutosha, niwaombe kuziondoa kesi zote ambazo hatuna uhakika wa kushinda, ni kupoteza fedha na muda kuendesha kesi ambazo mwisho wake wenyewe tunaona hatutoshinda.

Maelekezo mengine ni kwamba TAKUKURU iharakishe uchunguzi ambao Rais Samia aliagiza ufanyike kwenye Mamlaka ya Bandari nchini TPA, lakini pia iongeze juhudi za haraka kufikisha kesi za rushwa mahakamani kwa sababu hakuna kesi nyingi zilizopelekwa mahakamani badala yake kumekuepo na majadiliano nje ya mahakama," Amesema Mchengerwa.

Ametoa pia onyo kwa maafisa utumishi wote nchini kuhakikisha wanasimamia na kutatua changamoto za watumishi nchi na yeyote ambaye atashindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo hatosita kumuagiza Katibu Mkuu Utumishi kumuondoa kwenye nafasi hiyo.

" Haiwezekani watumishi wapate changamoto kwenye nafasi zao halafu kuna Maafisa Utumishi, niwatake maafisa utumishi wote kushughulika na changamoto za watumishi nchini na atakayeshindwa tutamuondoa kwenye nafasi hiyo," Amesema Mchengerwa.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

1/Post a Comment/Comments

Post a Comment

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2