RAIS SAMIA AWAONYA WANAOTUMIA MITANDAO YA KIJAMII KUTOA TAARIFA ZA KUCHONGANISHA KUHUSU KIFO CHA HAYATI MAGUFULI ...ASEMA WANAWAFUATILIA | Tarimo Blog


* Atoa ruhusa mawaziri wake kukosolewa Bungeni, atoa hofu waliyo na hofu dhidi yake

* Awahakikishia Watanzania kusimamia yote yaliyokuwa yanasimamiwa na Magufuli

Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV

RAIS wa Jammhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa onyo kwa baadhi ya watu ambao wanaandika na kutoa taarifa za uchochezi, hivyo amewataka kuacha mara moja tabia hiyo kwani ipo siku watapatikana na kama wanaona hatawapatikana basi wamuogope Mungu.

Ametoa onyo hilo leo bungeni Mjini Dodoma wakati analihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni mara ya kwanza kulihutubia Bunge hilo tangu awe Rais kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dk.John Magufuli aliyefariki Dunia Machi 17 mwaka huu.

Rais Samia amesema "Katika mitandao huko nimekuwa nikifuatilia na kuona yanayoendelea,  ukweli hayafutahishi kwani ni mambo yanayochanganisha wananch. Dini zetu zinasema kila nafsi itaonja umauti, wanatumia njia ambazo wanajua wao kutoa lugha za uchonganishi.

"Kuna watu wanahatarisha amani, wanasema fulani na fulani wanahusika kifo cha mpendwa wetu Dk.Magufuli, waache kuleta uchonganishi, kama wanaona hatutawapata kwasababu wanatumia njia ambazo hatuna uwezo nazo kuwamata ,ipo siku  tutapata,tunawafuatilia.Lakini kama wanaamini hatutawapata basi warudi kwa Mungu wao, wajiulize ingekuwa wao wangekubali kufanyiwa hivyo."

Amefafanua kwamba anachofahamu ni kwamba kifo cha Hayati Magufuli kimetokana na maradhi ya udhaifu katika moyo ambayo yamemsumbua kwa zaidi ya miaka 10 na ndio chanzo cha kifo cha mpendwa wetu."Kama kuna mtu anazo taarifa aje atueleze tutamsikiliza lakini wale wanaotumia mitandao kuchonganisha waache mara moja."

Wakati huo huo, Rais Magufuli ametumia Bunge hilo kueleza kwamba wabunge wanatakiwa kuwakosoa mawaziri wake pindi watakapokuwa wanapeleka hoja bungeni ."Mawaziri wangu wakosoeni vikali hapa bungeni lakini.mkosoe kwa lugha za kibunge."

Aidha amewaonya wale wote ambao wameanza kufanya ubadhirifu wa fedha za umma katika mashirika ya umma tangu kumeibuka wimbi la wizi tangu kilipotokea kifo cha Hayati Magufuli."Niwaonye wale wote wanaofuja fedha za umma, nakemea uvivu,uzembe na kamea wanaokwepa kodi maana kuna watu wanaamini baada ya kuondoka Rais Magufuli ameondoka na yale aliyokuwa akiyasimamia.

"Kuna baadhi ya mashirika wizi umeanza, kuna mashirika yalikuwa yanakwenda vizuri lakini sasa wanarudi nyuma.Niwahakikishie tutasimamia yote kama alivyokuwa akisimamami Hayati Magufuli,hatutarudi nyuma, "amesema Rais Samia.

Wakati huo huo amesema katika historia ya nchi yetu ni mara ya kwanza kupata Rais mwanamke, na kwamba kuna watu wanahisi atashindwa kutekeleza yote aliyosema." Mungu hakuumba ubongo dhaifu kwa mwanamke  na wala hakuumba  ubongo imara kwa mwanaume, umahiri wa ubongo unatokana na malezi ambayo umekulia, nimelelewa vizuri.

"Sina shaka na nafasi hii, si mgeni kwenye uongozi wa Serikali na yote niliyosema hapa siendi kufanya kazi peke yangu bali nakwenda kufanya  na Watanzania wote,"amesema Rais Samia wakati anahitimisha hotuba yake iliyochua saa 1:30 akitoa muelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita.
Mwisho



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia Bunge kutoa mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita leo Aprili 22, 2021 Jijini Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi mara baada ya kulihutubia Bunge leo Aprili 22, 2021 Jijini Dodoma.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (Katikati)akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi mara baada ya kulihutubia Bunge leo Aprili 22, 2021 Jijini Dodoma. Wa pili kushoti ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mhe. Ali Hassan Mwinyi, wa pili kushoti ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, wa kwanza Kushoto ni Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango na wa kwanza kulia ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Mwinyi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (wa tatu kulia walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Ulinzi na Usalama mara baada ya kulihutubia Bunge leo Aprili 22, 2021 Jijini Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiteta jambo na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (Kulia) mara baada ya kulihutubia Bunge leo Aprili 22, 2021 Jijini Dodoma.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2