Wakulima waaswa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa mnyauko wa mahindi ulioanza kuathiri eneo la Bonde la Eyasi. | Tarimo Blog

 

 Na Woinde Shizza, Michuzi Tv

Ugonjwa huo wenye tabia ya kudumaza mahindi na kusababisha mnyauko  unasambaa kwa njia ya maji, mvua, upepo vifaa vya kilimo ambavyo vimetumiwa katika shamba liloathirika na kwenda kutumika sehemu nyingine  bila kusafishwa vizuri.

Tatizo hilo limebainika katika ziara ya mkuu wa wilaya ya karatu Abbas Kayanda pamoja na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama walipotembelea shamba la  taasisi ya Magereza ambalo kiasi cha hekari kumi na tano zimeharibika kutokana na kuathiriwa na ugonjwa wa mnyauko wa mahindi MLND (Maize necrotic diseases). 

shamba lililotembelewa  walipanda mahindi kwa kutumia mbegu aina ya m seed co 513 na  mahindi hayo yaliyopandwa kuanzia mwezi wa kumi yameathirika sana na ugonjwa wa mnyauko wa mahindi ukilinganisha na mahindi ambayo yalipandwa kabla mvua kuanza kunyesha.

 Akiongea katika ziara hiyo Kayanda alihimiza elimu kutolewa kwa wananchi katika mikutano ya hadhara ya kijiji na ngazi ya kitongoji, ili kuwaelimisha wananchi juu ya ugonjwa wa mnyauko wa mahindi.

Alisema wananchi wakijengewa uelewa inakuwa ni rahisi kukabiliana na ugonjwa huo, kwa sababu watalima kwa kufuata maelekezo ya maafisa kilimo.

Aidha alimuelekeza Afisa kilimo wa wilaya kuandaa kikao cha wadau wa kilimo kitakachohusisha mawakala wa mbegu za kilimo na pembejeo, wakulima na wataalamu wa kilimo ili kujadiliana na kuja na mapendekezo yatakayosaidia serikali kukabiliana na tatizo hilo la  ugonjwa wa mnyauko wa mahindi shambani.

Afisa kilimo wa kata ya Baray  Johnson Christian Ishengoma alisema ili kukabiliana tatizo hilo  la  mnyauko wa mahindi, wakulima wanapaswa kuwahi kupanda mazao ardhini katika kipindi cha mwezi tisa au kabla kwa sababu virusi wanaosababisha mnyauko wa mahindi wanakuwa dhaifu na wamefubaa hivyo hawawezi kushambulia mmea wa mahindi. 

Aliongeza kusema katika kipindi cha kupanda mkulima anapaswa kupuliza dawa ya kuuwa wadudu kama utitiri na kimamba ili kuwezesha kukinga mmea na wadudu wanaoathiri mimea ya mahindi.

Ishengoma alisema mahindi yanayopandwa wakati mvua zimeshaanza kunyesha, yanaathirika sana na ugonjwa wa mnyauko wa mahindi kwa sababu virusi vinakuwa vinafanya kazi (active) na mkulima hugundua mmea umeathirika wakati mhindi unapokuwa katika kimo cha kwenye magoti hivyo inakuwa ni vigumu sana kukabiliana na athari za kirusi huyo kwa sababu mpaka sasa hakuna dawa ya kuwauwa.

Ishengoma alisema njia nyingine ni kushauri wakulima kupumzisha shamba kwa kupanda mazao mengine kwa muda wa miaka mitatu ili virusi vidhoofu na vipoteze uhai ardhini ,hiyo inasaidia kulipa shamba rutuba lakini inaondoa virusi hao wanaokausha mahindi kwa sababu hawana uwezo wa kuathiri mazao mengine.

Ishengoma alibainisha shamba lililoathiriwa na virusi vya ugonjwa wa mnyauko mahindi mabua yake yanapaswa kuchomwa na kuteketezwa, pia hayafai kulisha mifugo wa sababu yanasababisha kansa kwa wanyama,na  hata mnyama atakayechinjwa aliyekuwa akitumia mabuaa mahindi yaliyoathirika kwa kunyauka yanaathari za moja kwa moja kwa binadamu.

Alisema tunahitaji kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa huu, hata kwenye vifaa au nguo ambazo mkulima atafanya nazo shughuli za kuteketeza mahindi yaliyoathirika kwa ugonjwa huu lazima asafishe kwa maji na sabuni ili asisambaze vimelea hivyo kwenye shamba jingine.




Mkuu wa wilaya ya karatu Abbas Kayanda akiangalia  shamba la taasisi ya magereza lililopo katika  eneo la Bonde la Eyasi  wilayani humo  lililoathiriwa na ugonjwa wa mnyauko wa mahindi (picha na Woinde Shizza,Arusha )

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2