Na Zainab Nyamka, Michuzi Tv
WANANCHI wa Kata ya Kongowe Kibaha Mkoani Pwani kuendelea kunufaika na mradi wa maji wa kiwanda cha kuchakata nyama TanChoice uliokamilika Mwaka jana ukiwa na uwezo wa kuzalisha maji Lita Milion 12 kwa siku.
Mradi wa Maji wa TanChoice umetekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa thamani ya bilion 1.14 fedha za ndani.
Akitoa taarifa hiyo, Meneja wa Dawasa Mkoa wa Kihuduma Kibaha Alpha Ambokile amesema mradi huo uliweza kukamilika mapema mwaka jana na kuanza kutoa huduma kwenye kiwanda hicho.
Amesema, Dawasa walilaza bomba kubwa la inchi 10 kwa urefu wa Km 12 kutoka barabara kubwa linalotokea Ruvu Juu ili kupeleka maji kwenye kiwanda hicho cha kuchakata nyama.
"Mradi huu ni mkubwa, umegharimu Bilion 1.14 zikiwa ni fedha za ndani na Dawasa tumelaza bomba la inchi 10 kwa urefu wa Km 12 kutokea barabarani hadi kiwandani,"amesema
Ambokile amesema, katika mradi huo umeweza pia kuwanufaisha kampuni ya Yapi Merkez wanaojenga mradi wa tren ya mwendo kasi SGR eneo la Msoga ambao awali walikua wanayafuata maji mbali.
Amesema, mbali na hao pia wananchi wa Kata ya Soga mtaa wa Dengwa wameweza kunufaika na kwa sasa Dawasa wapo katika hatua za mwisho za kupeleka huduma ya maji kwa wananchi wa Kata ya Kongowe Mtaa wa Kigelo kupitia bomba hilo.
Akizungumza na Michuzi Blog,Meneja uzalishaji wa Kiwanda cha kuchakata nyama TanChoice, Ahmed Jama amesema wanafurahia huduma inayotolewa na Dawasa kwani hawana chanzo kingine cha maji wanachokitumia katika uzalishaji wa kila siku.
Jama amesema, walianza uzalishaji mwezi Agosti mwaka jana na kazi inaendelea kwa kasi kubwa sana na wamekuwa wanatumia maji ya Dawasa kwa wakati wote na pindi maji yanapokosekana huwa wanasimamisha uzalishaji.
"Kuna changamoto mbalimbali zipo na Meneja wa Dawasa Alpha amekuwa msaada mkubwa sana kwetu tumekuwa tunapata taarifa kama kuna matengenezo au hitilafu ya umeme kwani maji yanapokosekana yale yanayokuwa katika matanki yetu yanafanya uzalishaji mmoja tu," amesema.
Kiwanda cha Tanchoice kilianza uzalishaji mwaka 2020, na Kiwanda hiki kinatumia teknolojia ya kisasa, kitakuwa na uwezo wa kuchakata ng’ombe 1,000 na mbuzi na kondoo 4,500 kwa siku, tayari kimezingatia viwango vya kitaifa na kimataifa ambavyo husimamiwa na Shirika la Viwango nchini (TBS) ikiwa ni pamoja na mfumo wa usimamiaji wa usalama wa chakula ISO 22000 na usimamizi wa mfumo wa ubora ISO 9001.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment