Charles James, Michuzi TV
KATIBU MKUU Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbas amesema katika kutambua mchango wa sekta ya sanaa nchini serikali imeanzisha mfuko wa maendeleo ya sanaa na utamaduni lengo likiwa ni kuzipa sekta hizo mbili nguvu.
Kauli hiyo ameisema jijini Dodoma wakati akizungumza na Viongozi, Watumishi wa Kampuni ya Multichoice Tanzania ambao ndio wamiliki wa king'amuzi cha DSTV katika Iftari iliyoandaliwa na kampuni hiyo na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo Wabunge, Wasanii na wadau wengine wa habari na sanaa.
Dk Abbas amesema kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii wizara yenye dhamana ya sanaa na utamaduni kwenye bajeti yake ya mwaka huu kutakua na bajeti ya maendeleo ya sanaa ambapo amewaomba wabunge kuipitisha ili ikawe tija kwa wasanii nchini na Taifa kwa ujumla.
" Serikali yenu ni sikivu na inathamini mchango wa sanaa katika ukuaji wa uchumi wa Nchi yetu, na ndio maana kwa kulitambua hilo tumeanzisha mfuko huu ambao huko awali haukuwahi kuwepo, lengo letu ni kuona sanaa ya nchi yetu na wasanii kwa ujumla mnasonga mbele.
Kupitia mfuko huo wa maendeleo ya sanaa, tumepanga kuwapatia wasanii wetu mitaji ya kuwawezesha kutengeneza kazi nzuri kulingana na bajeti zao ili kuweza kupata kazi zilizo bora na za Kisasa, lakini pia kupitia mfuko huo tutakua tunatoa mafunzo kwa wasanii wetu," Amesema Dk Abbas.
Dk Abbas pia ameipongeza kampuni ya Multichoice kupitia king'amuzi chake cha DSTV kwa namna ambavyo imekua na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa sanaa nchini lakini pia wakiwa vinara kwenye michezo na kijamii.
" Hakika DSTV ni vinara katika ukuzaji wa filamu zetu, tunaona namna ambavyo mmefanya mapinduzi makubwa na kukuza sanaa yetu, mmegawa ajira nyingi kupitia mpango wenu wa kuonesha filamu za hapa nyumbani lakini pia mmechochea kuipa thamani kubwa sanaa yetu, nyie ni vinara, " Amesema Dk Abbas.
Amesema anafahamu kuna changamoto mbalimbali zinazowakabili sekta ya sanaa lakini ni imani yake kwamba mpaka kufikia mwakani watakua wametatua changamoto nyingi kama siyo kuzimaliza kabisa.
Kwa upande wake Mkuu wa Masoko wa Multichoice Tanzania, Baraka Shelukindo amesema kupitia tamthilia kama Huba, Juakali, Pazia na Slay Queen wamefanya familia nyingi zirudishe upendo huku akiahidi kuendelea kuonesha filamu za Tanzania kwa wingi zaidi na kuchochea kukua kwa sanaa na wasanii.
" Kupitia Chanel yetu ya Maisha Magic tumetoa ajira nyingi sana, siyo kwa wasanii tu bali kupitia tamthilia nilizozitaja tumewapa ajira vijana wengi kwenye eneo la Camera, uandishi wa muswada, uzalishaji na hata uandaaji, ni ahadi yetu kwa Serikali na watanzania kwamba DSTV itaendelea kuwalisha kile kilicho bora.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment