Charles James, Michuzi TV
SERIKALI imesema kufikia mwaka 2022 itakua imekamilisha mchakato wa kuweka nishati ya umeme kila Kijiji Nchi nzima na baadhi ya vitongoji.
Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja alipokua akifungua mkutano wa pamoja baina ya Wakala wa Nishati Vijijini REA na Wafadhili wa mradi huo kutoka Norway, EDPG wenye lengo la kuangalia maendeleo ya miradi inayotekelezwa na Wakala huyo nchini.
Mhandisi Masanja amesema kikao hicho kinalenga kukumbushana nia ya REA kupeleka umeme kila Kijiji pa pamoja na kukagua miradi hiyo pamoja na kujadili mpango kazi wa kutekeleza miradi ya umeme Vijijini.
" Nchi yetu imepiga hatua kubwa Sana katika kusambaza umeme, ukiangalia mwaka 2015 ni vijiji takribani 2,000 pekee vilivyokua na umeme, lakini leo tunazungumzia vijiji 10400 vina umeme Kati ya 12,000 nchi nzima.
Umeme ni nyenzo muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Nchi yetu, ukiangalia maeneo mengi yenye umeme yamepiga hatua za kimaendeleo, tunaendelea na juhudi zetu za kuhakikisha tunafikia maeneo mengi zaidi ili kuweza pia kufungua fursa za kiuchumi kwenye maeneo hayo," Amesema Mhandisi Masanja.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Julius Bundala amesema tayari wameanza mzunguko wa pili wa awamu ya tatu ambapo miradi hii ya umeme vijijini kwa asilimia 90 inatekelezwa kwa fedha za serikali huku asilimia 10 pekee zikitoka kwa wafadhili.
" Kupitia kikao hiki na wadau wetu hawa tutajadili bajeti na mkakati wa kuweza kutekeleza miradi yetu na tunaamini wafadhili wetu hawa watatusaidia kutekeleza miradi hii kwenye baaedhi ya maeneo.
Hadi kufikia Desemba 2022 vijiji vyetu vyote nchini vitakua vinawaka umeme na sasa tutakua na kazi ya kuanza kuwasha umeme kwenye kila kitongoji, lengo letu ni kuifanya Tanzania yenye umeme wa kutosha ili tuweze pia kuchochea ukuaji wa uchumi wetu," Amesema Bundala.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Wateja wa REA, John Zolotu ametoa rai kwa wateja wote wa REA kuhakikisha wanatumia mafundi wanaotambulika na Tanesco wakati wakufanya 'wiring' kwenye nyumba zao ili kuepuka vishoka wanaoweza kuwafanyia kwa bei kubwa.
" Sisi Kama REA hatutaki kuona mwananchi ambaye anaishi nyumba isiyo na umeme, na hiyo ndio maana tumeanza na umeme vijijini kisha vitongoji vitafuatia, rai yangu kwao ni wahakikishe wanatumia mafundi wanaotambulika pindi wanapofanya wiring kwenye nyumba zao ili kuepuka vishoka ambao wanawachaji bei kubwa," Amesema Zolotu.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment