HOTUBA YA AFISA MTENDAJI MKUU WA LSF - SIKU YA UHURU WA HABARI ARUSHA TANZANIA | Tarimo Blog

Afisa Mtendaji Mkuu wa Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng'wanakilala akizungumza wakati sherehe z maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari zinazofanyika kitaifa leo Mei 03, 2021 Jijini Arusha.

Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Mkuu Wa Mkoa wa Arusha.
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Technologia ya Habari.
Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Muwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa nchini Tanzania.
Mheshimiwa Balozi wa Sweden nchini Tanzania.
Waandaaji wa shughuli za maadhimisho ya kidunia ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari.
Wawakilishi wa sekta ya habari nchini Tanzania.
Ndugu waandishi wa habari.
Itifaki imezingatiwa

Kwanza, ningependa kuwashukuru sana wadau wote mliokusanyika hapa kwa ajili ya kuadhimisha siku hii maalum ya uhuru wa vyombo vya habari. Na sisi kama LSF tunajisikia fahari kuwa sehemu ya maadhimisho haya.

Ndugu zangu,
Sote tunatambua kuwa vyombo vya habari vimekuwa ni muhimili mkubwa katika maendeleo popote pale duniani kwa kutoa taarifa zinazolenga kujenga misingi ya uwajibikaji katika jamii kwa kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha.

Wakati mwingine vyombo vya habari husimamia mamlaka za kiserikali na kuibua masuala mbalimbali yaliyojificha kwa maslahi mapana ya wananchi wa kawaida.

Kwa miaka 10 sasa LSF imekuwa ikifanya kazi ya kuwezesha upatikanaji wa haki nchini Tanzania, na vyombo vya habari vimechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio tunayoyafikia.

LSF tunawezesha upatikaaji wa haki kwa watanzania nchi nzima kila mkoa na kila wilaya Tanzania bara na Zanzibar huku tukitilia mkazo kwa wanawake ambao ndio waathirika wakubwa. Kwa mwaka tunawafikia watu zaidi ya milioni 6 kwa kuwapatia elimu juu na maswala mbalimbali ya sheria, elimu inayowawezesha kudai haki zao pale wanapozikosa.

Pia tunawezesha utatuzi wa kesi na migogoro mbalimbali bure bila gharama yoyote na takribani watu 99,000 wanafikiwa kila mwaka

Tumeweza pia kufanya kazi katika kuanzisha na kuboresha sera na sheria mbalimbali nchini. Hapa tunafanya kazi kwa karibu kwa kushirikiana na serikali.Na tunafanya kazi katika maeneo mengi kwani haki inagusa maeneo mbalimbali.

LSF ni wadau wakubwa wa vyombo vya habari na vimeleta tija kubwa katika kuwezesha wananchi kutambua na kudai haki zao pale zinapopotea kwa manufaa yao na jamii kwa ujumla.

Vyombo vya habari vimesaidia kukemea vitendo vya ukatili wa kijnisia, ukandamizwaji wa wanawake na watoto wa kike lakini kukemea vitendo vya uvunjifu wa amani.

Tunafanya kazi karibu na UNESCO lakini pia tuna makubaliano ya mashirikiano na Mtandao wa Radio za Kijamii Tanzania (TADIO) kwa miaka 3 na ushirikiano huu umeleta tija kubwa sana

Ndugu zangu
Leo ni siku muhimu kwa wanahabari nchini.

sisi kama shirika tunatambua kuwa Uhuru wa habari umelindwa kikatiba katika ibara ya 18 ya Katiba ya Tanzania pamoja na Mikataba ya Kimataifa ambayo Tanzania imeiridhia.

Na tunaamini ili kuwa na jamii yenye usawa na ushirikishi katika maendeleo ya kijamii na uchumi ni muhimu kupata taarifa sahihi zitakazowezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi.

Hivyo nachukua fursa hii kuipongeza serikali kwa kuona kuna umuhimu wa kuendelea kulinda uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Tunajua kuwa bado kuna sheria zinazoonekana zinahitaji marekebisho kwa ajili ya ustawi wa vyombo vya habari. Ni muda muafaka sasa kwa serikali kutazama namna bora ya kuziboresha sheria hizi ili kujenga mazingira rafiki ya waandishi.

LSF tunaahidi kushirikiana na serikali pamoja na wadau mbalimbali katika kuwezesha mchakato wa kuwezesha mabadiliko hayo.

Mwisho kabisa, napenda kuwapongeza waandishi wa habari kwa kazi nzuri mnayoifanya katika kuhabarisha umma juu ya maswala mbalimbali.

Tunapoendelea kuadhimisha siku hii muhimu leo napenda kusisitiza kuwa kupata taarifa ni haki ya msingi ya binadamu.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2