TIA YAPEWA MAFUNZO YA UTAWALA BORA, YAJIPANGA KUFUNGUA MATAWI KOTE NCHINI | Tarimo Blog





Wajumbe wa Bodi ya Ushauri (MABU,) na watendaji wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) pamoja na mameneja wa kampasi hiyo kutoka mikoa sita nchini wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mafunzo maalumu ya Utawala bora yanayotolewa na Taasisi ya Institute of Directors kwa siku mbili, Leo jijini Ilala.
Mafunzo yakiendelea.
Kaimu mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Dkt. Modest Assenga akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mafunzo ya siku mbili ya Utawala bora yanayotolewa kwa wajumbe wa Bodi ya ushauri (MABU)  watendaji wa Taasisi  ya Uhasibu Tanzania (TIA) na Mameneja wa Kampasi hiyo ktoka matawi sita nchini  ili kuimarisha utawala bora wa maendeleo pamoja na kujenga maslahi kwa Serikali na watanzania kwa ujumla leo jijini Ilala.
Mwenyekiti wa Bodi ya ushauri (MABU,)Said Chiguma akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mafunzo hayo yaliyotolewa na Taasisi ya Wakurugenzi (Institute of Directors) na kueleza kuwa wanategemea matokeo chanya ya kujenga Taasisi hiyo mara baada ya mafunzo. Leo jijini Ilala.

 

KATIKA kuimarisha utendaji na sekta ya utawala Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA,) Wajumbe wa Bodi ya Ushauri (MABU) pamoja na mameneja wa kampasi za taasisi hiyo kutoka mikoa sita nchini wamepewa mafunzo maalumu ya Utawala bora yaliyotolewa na Taasisi ya wakurugenzi (Institute of Directors.) Ambapo  viongozi hao kila mmoja kwa nafasi yake wametakiwa kuwajibika ili kuyafikia malengo yaliyowekwa na Taasisi hiyo adhimu nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Ilala mkoani Dar es Salaam  mara baada ya mafunzo hayo Kaimu mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA)  Dk. Modest Assenga amesema mafunzo hayo yamelenga kuimarisha maendeleo ya Taasisi hiyo pamoja na kujenga maslahi bora kwa serikali na watanzania kwa kuzingatia ushirikiano na kutimiza wajibu kwa bodi ya ushauri ya Taasisi na Utawala wa Taasisi.

Amesema katika mafunzo hayo watabadilishana uzoefu ili kuyafikia malengo ya Taasisi hiyo hasa kwa kusimamia rasilimali za Taasisi pamoja na kutoa ushauri kwa Serikali.

''Taasisi hii tangu kuanzishwa kwake imekuwa ikitekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo kutoa elimu, kufanya tafiti mbalimbali za kiuchumi na biashara pamoja na kutoa ushauri kuhusiana na masuala mbalimbali ya kiuchumi na biashara, Hivyo kupitia mafunzo haya tunaamini tutapiga hatua zaidi na kuipeleka Taasisi yetu mbali zaidi.''

Aidha kuhusiana na changamoto zinazoikumba Taasisi hiyo Assenga amesema kuwa, Licha ya kuwepo kwa Taasissi za namna hiyo TIA imejipanga kwa kutumia silaha ya kutoa kozi zitakazowawezesha wahitimu kujiajiri na sio kutegemea kuajiriwa moja kwa moja.

''TIA ina matawi mengi nchini na tumejipanga katika kukabiliana na ushindani na hiyo ni pamoja na kuendelea kusambaa kupitia matawi ya Taasisi hii kote nchini.'' Amesema.

Kuhusiana na suala la wahasibu wengi kutokuwa waaminifu katika maeneo wanayofanya kazi Assenga amesema, Taasisi hiyo imekuwa ikiwajenga wanafunzi kwa nidhamu ya juu katika usimamizi wa fedha na kusema kuwa ni nadra kusikia wahitimu wa Taasisi hiyo wakikutwa na hatia ya matukio ya ubadhilifu wa fedha katika maeneo wanayofanya kazi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya ushauri wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA,) Said Chiguma amesema mafunzo hayo ya siku mbili yamefika wakati muafaka wakati Taasisi hiyo ikielekea kupata bodi mpya  itakayoshirikiana na Utawala ili kuyafikia malengo ya Taasisi pamoja na kubadilishana uzoefu na ujuzi.

Amesema mafunzo hayo yaliyowakutanisha na wakuu wa matawi sita ya TIA, viongozi wa utawala na bodi ya ushauri ni katika kufanikisha malengo yaliyowekwa na Taasisi hiyo na kusema kuwa  wafanyakazi wategemee viongozi imara na wanafunzi wategemee kupokea mafunzo kwa haki na  utaratibu uliowekwa pamoja na utatuzi wa changamoto zinazowakabili.

Mafunzo hayo yamehudhuriwa na wakuu wa matawi ya Taasisi hiyo kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Kigoma, Singida na Mtwara.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2