Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar
Kufunguliwa kwa Kituo cha Uendeshaji Huduma za Dharura za Afya ya Jamii Zanzibar (ZPHEOC) chenye kiwango cha Kimataifa ni suluhisho sahihi la maradhi ya mlipuko nchini.
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui ameeleza hayo katika hafla ya ufunguzi wa Kituo cha Uendeshaji Huduma za Dharura za Afya ya Jamii kilichopo Lumumba Mjini Zanzibar ambapo mgeni rasmi alikuwa Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dk. Donald Wright.
Waziri Mazrui amesema Zanzibar ikiwa ni sehemu ya dunia inaunganisha watu wa mataifa tofauti kwa shughuli mbali mbali za kiuchumi na matembezi, hivyo maradhi ya mripuko yanaweza kutokea na kuathiri wananchi kwa kipindi kifupi.
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto amesema kituo hicho kilichoanzishwa kwa msaada kutoka Kituo cha Udhibiti wa Maradhi cha Marekani (CDC), Shirika la Afya Duniani (WHO) na Taasisi ya Global Fund kwa sasa kishughulikia uchunguzi wa maradhi ya Covid 19.
“Kituo hichi kitakachofanyakazi kwa saa 24 kwa siku kitaongeza uwezo wa wataalamu wa afya ya jamii kudhibiti milipuko ya maradhi na kushughulikia dharura za kiafya kwa uratibu ulio mzuri zaidi na kwa ufanisi ,“alisema Waziri Nassor Mazrui
Alilishukuru Shirika la WHO, Kituo cha Udhibiti wa Maradhi cha Marekani (CDC), na Taasisi ya Global Fund kwa kukifanyia matengenezo makubwa kituo hicho na kukipatia vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa maradhi mbali mbali na vitendeakazi.
Katika ufunguzi wa kituo hicho, Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dk. Donald Wright ametangaza msaada mpya wa Dola za Kimarekani milioni 1.2 kwa Wizara ya Afya ya Zanzibar kusaidia jitihada za kubaini na kushughulikia milipuko ya maradhi, hususan janga la COVID-19.
Dk. Donald amesema lengo kuu la ZPHEOC ni kuendesha Huduma za Dharura za Afya ya Jamii Zanzibar ili kushughulikia kikamilifu na kwa ufanisi vitisho kwa afya ya umma.
Balozi wa Marekani amesema mbali na kusaidia jitihada za Wizara ya Afya ya Zanzibar za kudhibiti milipuko ya maradhi kubaini na kuchukua hatua za kuzuia kuenea kwa maambukizi, nchi yake inachangia pia kwa kutoa fungu jipya la kusaidia utoaji matibabu muhimu kwa wagonjwa, ikiwemo wale walioathiriwa na janga la COVID 19.
Meneja wa Kituo cha Uendeshaji Huduma za Dharura za Afya ya Jamii Dkt. Hussein Ame Haji akimpa maelezo Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Donald Wright baada ya ufunguzi rasmi wa kituo hicho katika eneo la Lumumba Mjini Zanzibar.
Mwakilishi wa WHO Zanzibar Dkt. Andemichael Ghirmay akitoa ahadi ya Shirika hilo kuendelea kushirikiana na Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto katika kuimarisha afya ya Jamii Zanzibar.
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui akitoa hutuba yake mara baada ya ufunguzi wa Kituo cha Uendeshaji Huduma za Dharura za Afya ya Jamii kilichopo Lumumba Mjini Zanzibar.
Balozi wa Marekani Dkt. Donald Wright katika picha ya pamoja na Viongozi na wafanyakazi wa Kituo cha Uendeshaji Huduma za Dharura za Afya ya Jamii kilichopo Lumumba Mjini Zanzibar.
Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Donald Wright akiwa na Mkurugenzi wa Hospitali ya Mnazimmoja Dkt. Msafiri Marijani alitembelea Hospitali Kuu ya Mnazimmoja Mjini Zanzibar. Picha na Makame Mshenga.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment