KAIMU Mkurugenzi Mkuu, Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Dkt. Jonas Kizima amesema utafiti wanaoufanya utasaidia kutatua changamoto za mbegu bora za malisho ya mifugo kwa wafugaji ili sekta ya mifugo iweze kuchangia vyema katika pato la Taifa.
Dkt.Kizima aliyasema hayo juzi mifugo katika kituo cha TALIRI Wilayani Mpwapwa, Mkoani Dodoma wakati akizindua majaribio ya aina za majani ambayo yanaweza kumaliza changamoto ya malisho hapa nchini.
Alisema ni kuhakikisha wanapata mbegu bora za malisho ya mifugo ambazo zitakazosaidia kutatua changamoto za upatikanaji wa malisho na zinazohimili mazingira yaliyopo .
“TARILI imeendelea kufanya Tathmini ya ubora, ustahimilivu na makuzi ya malisho ya mifugo yatakayofaa kwa chakula cha kutosha kwa ajili ya mifugo.
“Matokeo yoyote ya utafiti lazima yabadilishwe kuwa biashara kwa sababu wafugaji wakifanya ufugaji unaoendana na mazingira yao itawasaidia kutengeneza uchumi na kuwaongezea tija katika ufugaji wao,”alieleza.
Aliongeza kuwa tafiti zinazozifanya zinalenga kuimarisha mnyororo wa thamani wa mifugo ili mchango wa sekta ya mifugo uweze kuonekana katika uchumi wa kati,” alisema Dkt. Kizima
Dkt. Kizima alisema TALIRI imesambaza vituo vyake katika Kanda Saba nchini ili kuwa karibu na wafugaji kuwasaidia kutatua changamoto zao ili waweze kufanya ufugaji wenye tija.
Alisema vituo hivyo vipo katika Kanda ya Mashariki, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kati, Kanda ya Kusini, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Ziwa na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Naye, Mkurugenzi, Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani, Dkt. Angello Mwilawa alisema kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imezihamasisha Halmashauri zote nchini kuanzisha mashamba darasa ya malisho ili wafugaji waweze kujifunza na kupata mbegu bora za malisho kwa ajili ya mifugo.
“Tunawahimiza wafugaji kuona umuhimu wa kulima malisho ili yaweze kuwasaidia kupata lishe ya uhakika kwa mifugo yao na pia kwa kulima malisho kutawapunguzia migogoro ya mara kwa mara kati yao na wakulima,” alisema Dkt. Mwilawa.
Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (Mifugo) Dkt. Angelo Mwilawa(aliyevaa Koti Jeupe) akiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (Taliri), Dk Jonas Kizima wakikagua moja ya vitalu vilivyooteshwa mbegu za majani kwa ajili ya kulishia mifugo wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment