NITAKUA SEHEMU YA WATU WATAKAOSIMULIA HISTORIA ILIYOWEKWA NA RAIS SAMIA | Tarimo Blog

 Charles James, Michuzi TV

LIPI umewahi kulishuhudia na kuliingiza kwenye kumbukumbu zako kama jambo la kihistoria ulilowahi kulishuhudia?

Wapo watanzania wengi wameweke rekodi na historia katika Taifa hili, lakini rekodi ya Mama Samia Suluhu Hassan inabaki kuwa rekodi ya peke yake.

Miaka saba nyuma alitambulika na watu wa tabaka fulani la wasomi na wafuatiliaji wa mambo. Hakua na jina kubwa katika medani za kisiasa na kiuongozi kwenye Nchi hii.

Hakuna ambaye alimuona kama mtu mkubwa katika nafasi tatu za juu za Taifa letu, hata aliposhika nafasi ya kuwa Makamu Mwenyekiti kwenye Bunge la Katiba mwaka 2014 bado haikuonekana Kama kitu 'special' sana.

Kumbuka katika miaka mitano ya mwisho ya utawala wa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, Mama Samia alikua akihudumu kama Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira.

Wizara ambayo imekua ikionekana kama wizara 'soft' isiyo na mishemishe.

Kumbe tayari Mungu alishachora jina lake kwa muhuri wa moto kwenye historia ya Nchi yetu na leo tunapozungumza ni yeye ndie anaetusalimia kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa amekaa kwenye kiti chekundu kama Rais na Kiongozi Mkuu wa Nchi yetu.

Nani alimtabiri? Nani alimuona kama atakuja kuwa hapa alipo sasa? Ungeweza kuamini ipo siku Mama Samia atakua Rais wa Nchi hii? Rais Mwanamke?

Mungu ameamua kumnyanyua Mama Samia katika kundi la Wanawake wa Tanzania kuwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu. Tuipokee salamu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wote tuseme 'Kazi Iendelee'.

Kupitia Mama Samia, Mwenyezi Mungu ameamua kuwainua Mama zetu wa Tanzania katika kipindi ambacho hakuna aliyetegemea, nyakati ambazo Taifa limempoteza 'Baba' aliyekua Rais Dk John Magufuli, basi Mungu ameamua kulivusha Taifa kupitia Mama.

Na wote ni mashahidi nyumba zote ambazo zimelelewa na Mama pekee basi zimekua na mafanikio makubwa. Huu ni uthibitisho wa namna ambavyo Mungu ametoa nguvu kubwa kwa Wanawake na Mama zetu.

Nitasimulia namna ambavyo Mwenyezi Mungu amemnyanyua Mama Samia na kuweka rekodi zake tatu za kibabe na ambazo ninaamini itachukua muda mrefu kuvunjwa.

Ya kwanza ni ile aliyoweka mwaka 2015 alipopitishwa kuwa Makamu wa Rais wa kwanza Mwanamke akiwa Msaidizi namba moja wa aliyekua Rais Hayati Dk Magufuli, hadi umauti ulipomkuta Magufuli Machi 17 mwaka huu.

Machi 19 mwaka huu akaapishwa kuwa Rais wa Tanzania ikiwa ni kwa mujibu wa Katiba yetu ambayo inaelekeza kuwa Makamu wa Rais ndiye atakua Rais endapo Rais aliyepo madarakani atafariki duniani.

Hivyo Mama Samia akaweka rekodi nyingine ya kibabe ya kuwa Rais wa kwanza Mwanamke Tanzania lakini na Afrika Mashariki.

Na kwa kuwa utaratibu wa Chama cha Mapinduzi ambacho ndio kinaongoza Nchi ni kwamba Rais ndio anakua Mwenyekiti wa chama basi April 30 mwaka huu Rais Mama Samia akaweka rekodi nyingine ya tatu na kubwa ya kuwa Mwenyekiti wa kwanza Mwanamke wa CCM.

Lipi la kusema zaidi? Mwenyezi Mungu ameamua kumnyanyua Rais Mama Samia bila matarajio yake wala sisi sote.

Na Nchi iko salama ikiwa chini yake, Nchi ina amani na furaha ikiwa chini yake, Taifa linasonga na kuzungumza lugha moja tukiwa na Rais Samia. Chini ya Mama hakuna mwananchi yoyote aliyepata 'mhaho'. Tunampenda, tunamheshimu na tunamuamini. Na kazi inaendelea.

CCM wana amani chini yake, wapinzani wanamuamini, watanzania wanamsikikiliza na zaidi ameahidi kuiunganisha Tanzania na Dunia. Nini zaidi tunataka? Chapa kazi Mama, chapa kazi Rais.

Halafu nachokipenda zaidi kwa Rais Samia ni kwamba yeye ni 'Bi Mkubwa' siyo 'Mummy' siunajua tofauti ya Bi Mkubwa na Mummy? Bi Mkubwa mtoto ukila hela ya Bi Mkubwa utaitapika, hakuna madeko kwa Bi Mkubwa. Kwa Mummy mtoto akila hela anaambiwa 'Dont Worry Son, Its Okay'.

Samia ni Mama wa Kiafrika, nidhamu, utii na heshima ndiyo sehemu yake, tunakuamini Rais wetu na nikutakie majukumu mema kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ramadhan Mubarak.

0683 015145

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2