RAIS SAMIA ATAKA JESHI LA POLISI KUJIKITA KUTUMIA SHERIA KUDHIBITI MAKOSA BADALA YA KUZIGEUZA KITEGA UCHUMI | Tarimo Blog




 
Na Said Mwishehe, Michuzi TV

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kwamba Jeshi la Polisi nchini sharia zao zilizotungwa ni sheria za udhibiti , hivyo jeshi hilo lijielekeze zaidi katika kudhibiti makosa badala kutumia sheria zilizopo kuzigeuza kuwa kitega uchumi.

Amesisitiza sheria zilizopo zaidi zitumike kudhibiti kuliko kujikita kwenye ukusanyaji fedha na tozo nyingine huku akitumia nafasi hiyo kusisitiza umuhimu wa jeshi la polisi kutoa elimu inayohusu usalama barabarani pamoja na usalama wa mali zao.

Rais Samia amesema hayo leo baada ya kuzindua kiwanda cha Ushonaji cha Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam ambapo wakati akitoa hotuba yake amezungumzia masuala mbalimbali yanayohusu jeshi hilo, hivyo ametumia nafasi hiyo kueleza anawashakuru Polisi kwa vipindi vyao vya kutoa elimu kwa umma kuhusu mambo yanayohusu usalama barabarani na usalama wa raia.

“Ninawashukuru sana kwa vipindi vile kwa kuwa elimu inatoka lakini naomba muongeze jitihada ili wananchi wengi zaidi waweze kuwasikia ili kupunguza hayo, ni vema na najua kiwanda hiki pengine kimejengwa kwa fedha hizo ,lakini ni vema kama tukajielekeza kwenye kutoa elimu zaidi kuliko kutumia sheria kama vitega uchumi.

Aidha Rais Samia ametumia nafasi hiyo kueleza kwamba pamoja na pongezi ambazo amezitoa kwa Jeshi la Polisi katika kukabiliana na uhalifu lakini bado kuna changamoto za kiusalama.”Kama nilivyowahi kusema nikiwa Mlimani City wanaojihusisha na vitendo vya ujambazi na uhalifu wasijaribu kupima kina cha maji kwa kutaka kurejesha vitendo vya vitendo vya ujambazi hapa nchini.

“Nakupongeza IGP  Sirro baada ya kauli yangu ile pale Mliman City, Mei 8 mwaka huu ulikutana na Jeshi la Polisi ili kuweka mikakati ya kupambana na hali hiyo, ni matumaini yangu kuwa tutaona matunda ya mkutano huo ingawa bado tunasikia vijitaarifa taarifa hawa watu wanaendelea kubonyeza.

"Naomba muwe wagumu wanapobonyeza msibonyee, mliweza na hakuna sababu ya kurudi nyuma sasa hivi.Naomba sana Jeshi la Polisi mjipange vizuri kukabiliana na hao wanaotaka kuwajaribu na hii sio hapa Dar es Salaam ni nchi nzima,”amesema Rais Samia.

Akifafanua zaidi amesema kwamba hivi sasa hata katika kuteua au kutengua makanda wa Polisi wa mikoa, moja ya kigezo ambacho atakitumia ni jinsi gani anayeteuliwa au anayetenguliwa anaweza kukapabiliana na wahalifu nchini.”Na niwe mkweli  miongoni mwa vigezo ambavyo tutavitumia kuteua au kutengua makamanda wa mikoa ni udhibiti wa vitendo vya ujambazi ikiwemo wa kutumia silaha.

“Hii nayo itakuwa moja kati ya vigezo, najua IGP umeniletea majina kadhaa kwa ajili ya zile Kamisheni mbili ya Fedha na Lojistiki na ile Kamisheni nyingine lakini hiki kitakuwa moja ya kigezo ambacho nitatumia.”


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2