Na Said Mwishehe, Michuzi TV
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Samia Suluhu Hassan amezindua Kiwanda cha Ushonaji cha Jeshi la Polisi mkoani Dar es Salaam ambapo amsema uzinduzi wa kiwanda hicho unakwenda sambamba na sera ya Tanzania ya Viwanda huku akishuri majeshi mengine nayo kuanzisha miradi au viwanda ambavyo vitakuwa na shughuli tofauti na ushonaji.
Akizungumza leo Mei 18, 2021 , Rais Samia amesema hivi karibuni Bungeni wamepitisha mpango wa maendeleo wa miaka mitatu kwa ajili ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa ajili ya maendeleo ya watu, hivyo uzinduzi wa kiwanda hicho unaendana kabisa na kauli mbiu hiyo inayounga mkono nguvu ile sera ya Tanzania ya viwanda.
"Lakini pamoja na mradi huu nimemsikia IGP kuna mlolongo wa viwanda kadhaa na miradi mingi ambayo inapangwa kutekelezwa, nami naomba niwatie nguvu miradi hiyo itekelezwe kwa nguvu zote. Nimejulishwa kwamba mradi huu umejengwa kwa kutumia force account na kwa kiasi kikubwa kimeweza kupunguza gharama za ujenzi wa kiwanda hiki.
"Gharama halisi ni kama kiwanda kama kingejengwa na mkandarasi na Sh.bilioni 1.4 lakini gharama zilizotomika kwa kutumia force account ni Sh.milioni 666.4 , ni hatua nzuri na hongereni sana Jeshi la Polisi na ni imani yangu tutaendelea hata kwenye miradi mingine kutumia njia hii ili kupata ufanisi kuweka miradi mingi bila kupunguza sifa na ubora wa miradi na viwanda vinavyojengwa ,
"Mbali na kutoa ajira , kiwanda hiki kitazalisha ajira kitakuwa kikitengeza sare 125, 200 za askari na kitashona sare kampuni za majeshi mengine pamoja na kampuni za ulinzi binfsi, na ili muweze kufanya kazi hiyo lazima muoneshe mfano mzuri , wakati natembelea kiwanda nimeoneshwa sare ambazo zimeanza kushonwa na kudaliziwa na kiwanda hiki.
"Ni sare nzuri mnoo, hata mimi nimewekewa ya kwangu , sijui nitaivaa lini lakini kuna siku nitaivaa, lakini nami niungane nawe. IGP, vikosi vingine vya ulinzi vije kushona,"amesema Rais Samia na kuongeza kiwanda hicho kikuzwe vizuri ili majeshi mengine yashone sare zao hapo na kwamba kila.kikosi kiwe na shughuli yake.
Amefafanua vikosi vingine navyo viwe na viwanda ambavyo shughuli zake hazifanywi na kiwanda kingine, ili kila kikosi kiwe na shughuli yake inayofanyia kazi."Najua Magereza kwa mfano wamejikita kwenye bidhaa za ngozi, hivyo ni vema wakajikita katika bidhaa hizo za ngozi , pamoja na mambo mengine madogo madogo ya kilimo wanayofanya.
"Hii sio tu itaokoa fedha za serikali lakini itaongeza mapato kwa Jeshi la Polisi lakini la zaidi ni kwamba kiwanda hiki kitasaidia kudhibiti au uingizwaji holela wa sare za askari na hiyo kuimarisha usalama wa raia na mali zao.Sababu tunajua kuna visare sare vinatembea huko na watu wanavaa kutishia watu na kufanya mambo ambayo hayaeleweki.
"Nirudie tena kulipongeza Jeshi la Polisi kwa kujenga kiwanda hiki, nafarijika kuona kwamba vyombo vingne vya usalama kama nilivyosema JKT, JWTZ na vyombo vingine wanaviwanda vyao lakini kama nilivyosema nguvu kubwa tuweke hapa na wengine wa shughulike na mambo mengine , huu ndio muelekeo tunaoutaka,"amesema Rais Samia.
Ameongeza vyombo vya ulinzi vinayo nafasi kubwa ya kushiriki na kutoa mchango kwenye shughuli za kiuchumi , ikiwemo ujenzi wa viwanda bila kudumaza kazi za msingi za vyombo hivyo. " Nitumie fursa hii kuahidi kwamba Serikali itaendelea kuweka mazingira bora kwa ajili ya ustawi wa sekta ya viwanda ikiwemo kutoa vivutio mbalimbali vya kikodi na visivyo vya kikodi.
"Mbali na kushiriki kwenye shughuli za uchumi , jeshi la polisi lina dhamana kubwa ya kulinda usalama wa raia na mali zao, napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza askari wa jeshi la polisi kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya, sio siri kuwa hali ya usalama tuliyonayo sasa nchini inasimamiwa kwa kiasi kikubwa na jeshi la polisi pamoja na majeshi mengine"amesema.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment