Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) leo imezindua mradi wa maji wenye thamani ya shilingi 220m/- katika Kijiji cha Machochwe kilichopo wilayani Serengeti mkoani Mara ikiwa ni jitihada zake za kusaidia upatikanaji wa huduma ya maji salama kwa wananchi wa eneo hilo.
Mradi huo wenye uwezo wa kuhudumia watu 12,000, unahusisha uchimbaji wa kisima,ununuzi wa tanki la maji na pampu yenye uwezo wa kuvuta lita 7,500 kwa saa
Akizungumza wakati wa kukabidi kisima hicho, Mkurugenzi wa Mahusiano kwa Umma wa SBL John Wanyancha alisema kampuni hiyo kupitia mradi wa ‘Maji ni Uhai’ imesaidia uchimbaji wa visima vilivyosaidia upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mbali mbali ikiwamo Iringa, Kilimanjaro, Mwanza, Tanga, Ruvuma, Dar es Salaam, Pwani na Dodoma ikiwezesha upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa zaidi ya watu milioni moja.
Wanyancha alisema, mradi wa Machochwe hautasaidia tu kuboresha afya za wakazi wa eneo hilo, bali pia utaongeza uzalishaji mali kwa kuwa wasichana na akina mama hawatatembea tena umbali mrefu kutafuta maji na kuongeza kuwa utawapa wasichana muda zaidi wa kuhudhuria shule.
“SBL inayo sera inayolenga kuboresha maisha ya jamii zetu na Maji ni Uhai ni moja kati ya vipau mbele ambavyo vimeelezewa kwenye malengo ya kampuni yetu kuboresha maisha ya jamii inayotuzunguka,” alisema Wanyancha.
Mkurugenzi huyo alitaja vipaumbele vingine kuwa ni pamoja na Kutoa ujuzi kwa ajili ya Maisha, Utunzaji wa Mazingira na Unywaji wa Kiasi.
Zaidi, Wanyancha alisema SBL inao mpango wa kusaidia wakulima ambao kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita umefanikiwa kuwafikia na kuwasaidia wakulima 400 kwa kuwapatia msaada wa kitaalamu na kifedha hivyo kuweza kuboresha maisha yao na ya jamii zao
“Kupitia mpango huu, SBL imeweza kupata malighafi kwa ajili ya uzalishaji wake kutoka tani 0 hadi 17,000 zinazozalishwa na wakulima wa ndani jambo ambalo limesaidia ukuwaji wa kampuni na kuongeza kipato kwa wakulima pia,” alisema.
“Ukiachana na kuchangia uchumi wa nchi kupitia ulipaji kodi, SBL inatoa mchango wake kwa maendeleo ya nchi haswa kwa kusaidia upatikanaji wa maji safi na salama hapa nchini,” aliongeza.
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa mradi huo mkuu wa wilaya ya Serengeti Nurdin Babu aliishukuru kampuni ya SBL kwa kutoa msaada huo uliokuwa ukihitajika sana na kuongeza kuwa kampuni hiyo imekuwa mdau mkubwa wa maendelea hapa nchini.
Mkuu wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara Nurdin Babu, akimtwisha ndoo ya maji mkazi wa kijiji cha Machochwe Martha Marwa, baada ya kuzindua kisima kilichochimbwa kwa ufadhili wa Kampuni ya Bia ya Serengeti(SBL)katika kijiji hicho, mradi una thamani ya Sh 220 Milioni ambapo wakazi 12,000 watanufaika, wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Mahusiano kwa Umma wa SBL John Wanyancha.
Mkuu wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara Nurdin Babu akizungumza kwenye uzinduzi wa kisima kilichochimbwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) katika kijiji cha Machochwe, baada ya kuzindua mradi huo wenye thamani ya Sh 220 Milioni utakaonufaisha wakazi 12,000. Kushoto ni Mkurugenzi Mkazi wa Water Aid Anna Mzinga na Mkurugenzi wa Mahusiano kwa umma wa SBL John Wanyancha(kulia).
Viongozi wa kimila wa Machochwe wilayani Serengeti (walioshika fimbo)wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kuzinduliwa kwa kisima cha mji chenye thamani ya shilingi milioni 220 kilichochimbwa kwa uafadhili wa Kampuni ya Bia ya Serengeti. Kisima hicho kinaweza kuhudumia watu 12,000.
Mkurugenzi wa Mahusiano kwa Umma wa Kampuni ya Bia ya Serengeti(SBL) John Wanyancha akizungumza wakati wa kukabidhi kisima katika kijiji cha Machochwe mkoa Mara, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Nurdin Babu(wa pili kushoto), Mkurugenzi mkazi wa Water Aid Anna Mzinga(kushoto) na Katibu Tawala Wilaya ya Serengeti Kamara Cosmas(kulia).
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment