Charles James, Michuzi TV
SERIKALI ya Israel imetoa pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku wakiahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika sekta ya afya ambayo wamekua wakitoa mchango wao kwa muda mrefu.
Hayo yamesemwa na Balozi wa Israel nchini, Oden Joseph leo jijini Dodoma alipotembelea Taasisi ya Hospitali ya Benjamin Mkapa ambayo wamekua wakishirikiana nayo ikiwemo kuboresha huduma ya dharura.
Ushirikiano wa Israel na Hospitali ya Benyamin Mkapa ulianza mwaka 2018 kwa pande hizo mbili kusaini hati ya makubaliano ya kushirikiana na serikali ya Israel ilikubali kuboresha huduma ya dharura hasa ya wagonjwa majeruhi ambapo mpaka sasa kiasi cha Sh Bilioni 2 kimeshatumika kuboresha kitengo hiko.
" Nitoe pole kwa watanzania kwa kuondokewa na aliyekua Rais Dk John Magufuli na pia nimpongeze Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa kuwa Rais, nimuahidi kuendeleza ushirikiano uliokuepo baina yetu sote na kwamba serikali ya Israel itaendelea kutoa sapoti kwenye eneo hili la afya na maeneo mengine kwa manufaa ya pande zote mbili
Tumeombwa kutoa msaada wetu katika kuboresha eneo la vifaa tiba na kubadilishana uzoefu, tumelipokea hilo na kama tulivyoanza na eneo la huduma za dharura nina imani na hili pia tutafanikiwa," Amesema Balozi Oden.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel ameishukuru serikali ya Israel kwa namna ambavyo imeendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuwahudumia wananchi huku akimuomba kuendelea kutoa sapoti katika kuleta vifaa tiba, kubadilishana uzoefu na kuboresha miundombinu ya sekta ya afya.
" Niishukuru sana serikali ya Israel kwa kuendeleza ushirikiano huu katika sekta ya afya, niseme tu serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Sakis Suluhu Hassan imepanga kuboresha eneo la Uta lii wa Afya kwa kupokea wagonjwa wengi kutoka nje watakaokuja kutibiwa nchini, haya tutafanikiwa kwa kuzidi kuboresha sekta ya afya kama hivi," Amesema Dk Mollel.
Amesema maboresho haya ya sekta ya afya ni kuzidi kupunguza idadi ya watanzania wanaoenda kutibiwa nje ambapo sasa idadi imepungua hadi kufikia asilimia 95 na lengo likiwa kufikia asilimia 100.
Balozi wa Israel nchini, Oden Joseph akiwa na Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel pamoja na watumishi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa alipofika kuitembelea Hospitali hiyo.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment