Na Said Mwishehe, Michuzi TV
WASANII wa Filamu zaidi ya 200 kutoka mkoani Dar es Salaam wamefanya ziara ya kutembelea Hifadhi ya Msitu Asilia Pugu Kazimzumbwi uliopo wilayani Kisarawe mkoani Pwani wakiwa na lengo la kutangaza vivutio vilivyopo ndani ya Wilaya hiyo na nchi kwa ujumla.
Hifadhi hiyo ambayo inasimiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) imekuwa ikitembelewa na idadi kubwa ya watalii wa ndani na nje ya nchi kutokana na vivutio mbalimbali vilivyomo akiwemo panzi mwenye rangi za bendera ya Taifa la Tanzania, hivyo waigizaji hao wamepata fursa ya kutembelea hifadhi hiyo na kujiionea utalii uliopo.
Akizungumza leo wakati anawakaribisha wasanii hao wa tasnia ya uigizaji filamu, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo ameanza kwa kuwapongeza wasanii hao ambao wametoka kwenye wilaya zote tano za Mkoa wa Dar es Salaam na imani yake baada ya kutembelea vivutio hivyo watakuwa mabalozi wa kutangaza utalii wa Kisarawe ndani ya nje ya Tanzania.
"Tumepata neema kubwa ya kuvutia makundi mbalimbali ndani ya nchi yetu ya Tanzania , kuthamini rasilimali zilizopo Tanzania, kuthamini vivutio mbalimbali vilivyopo Tanzania na tumefurahi zaidi tumeweza kuvutia kundi kubwa zaidi la vijana kuweza kuona thamani ya kutalii katika vivutio vilivyopo katika nchi yao.
"Sisi mwanzoni mwa mwaka huu tumefanya kitu ambacho tulikita Kisarawe Ushoroba Festival , nawashukuru waandishi wa habari walishiriki vizuri, na tunajiandaa tena na tamasha kama hili kwa mwakani.Baada ya Kisarawe Ushoroba Festival tumeona hamasa ya watu mbalimbali kufika hapa imeongezeka mara dufu.
"Na kikubwa kweli, ujio wenu kama Chama cha Wasanii Mkoa wa Dar es Salaam ni uthibitisho tosha kwamba harakati zetu katika kutangaza vivutio vilivyopo ndani ya Kisarawe sasa imetiki, na sisi tunasema hili ambalo tumeanzisha ni kwa manufaa ya Taifa letu, watu wameitikia kwa wingi na wanajipanga wenyewe kuja kuangalia utalii wa ndani,"amesema Jokate.
Ameongeza huko nyuma maeneo hayo watu waliokuwa wanatembelea ni kutoka nje ya Tanzania na wengi wao walifika kwa ajili ya kufanya tafiti lakini sasa hivi TFS wameboresha miundombinu ndani ya msitu na sasa hata Watanzania wanavutika na kuona utalii uliopo ndani ya Tanzania, ndani ya Wilaya ya Kisarawe.
"Naamini ninyi ambao mmefika mtakuwa mabalozi, mtahamasisha watu wengine kutembelea vivutio vyetu, naamini hii sehemu itakuwa na watu mwaka mzima, wasanii ni kivutio , wasanii ni kioo cha jamii , wasanii mnamvuto kwani mkionekana sehemu mnavutia watu wengi zaidi.Mkija na watu wengine watakuja, wasanii wetu tunasema ahsanteni sana."
Kwa upande wake Mhifadhi wa Misitu Wilaya ya Kisarawe kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) Fred Ndandika amesema idadi ya watalii katika msitu huo imekuwa ikiongezeka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya kuboreshwa kwa miundombinu.
Amefafanua mwaka 2016/2017 idadi ya waliokuwa watu waliokuwa wamekwenda kutalii ilikuwa watalii 2,258 lakini kwa mwaka huu hadi sasa wameshatembelea watalii zaidi ya 4000."Na uzuri zaidi ya asilimia 80 ni watalii wa ndani.
Kuhusu kiingilio amesema kwa mujibu wa kanuni kwa mtanzania ni Sh.2000, mtoto Sh.1000 na kwa mtu ambaye si Mtanzania analipa Dola 10 ambayo ni sawa na Sh.25000 na baada ya kulipa kiingilio hicho atapa fursa ya kuona vivutio vyote vilivyomo ndani ya msitu huo.
Wakati huo huo Makamu wa Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania Nyakwesi Mujaya ametoa shukrani kwa Mkuu wa wilaya ya Kisarawe huku akifafanua kuwa unapozungumzia filamu basi unazungumzia utalii, hivyo kwenda kwao haitaishia kwenda kwenye mitandao bali wanaamini kufika kwao kutasaidia jamii kufahamu vivutio vilivyopo Kisarawe.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment