WATUMISHI TSC WAKUMBUSHWA MAJUKUMU YAO | Tarimo Blog
Mkurugenzi wa Idara ya Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Christina Hape, akiwasilisha mada kuhusu Kusudi la kuanzishwa kwa Tume hiyo wakati wa mafunzo kwa Kamati za Wilaya za TSC zinazoshughulikia ajira na maadili ya walimu zilizoko Kanda ya Ziwa, yaliyofanyika hivi karibuni jijini Mwanza.
Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Moses Chitama (kushoto) na Mkurugenzi wa Idara ya Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Christina Hape, wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa mafunzo kwa Kamati za Wilaya za TSC zinazoshughulikia ajira na maadili ya walimu zilizoko Kanda ya Ziwa, yaliyofanyika hivi karibuni jijini Mwanza.
………………………………………………………………………
Na Veronica Simba – TSC
Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) wamekumbushwa majukumu yao wanayopaswa kuyatekeleza katika utendaji kazi wao wa kila siku na kutakiwa kutoenenda kinyume nayo.
Majukumu hayo yalibainishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC, Christina Hape, wakati akiwasilisha mada kuhusu kusudi la kuanzishwa kwa Tume hiyo kwa wajumbe wa Kamati za Wilaya za Kanda ya Ziwa zinazoshughulikia ajira na maadili, kwenye mafunzo yaliyofanyika jijini Mwanza hivi karibuni.
Akielezea majukumu hayo, Mkurugenzi Hape alisema ni pamoja na kuwatumikia walimu kwa bidii, uaminifu na kwa kujituma katika masuala ambayo Serikali imeipatia TSC kwa mujibu wa sheria, ili kupunguza malalamiko ya walimu na kuwafanya watekeleze majukumu yao ya ualimu kwa furaha.
Vilevile, alisema kuwa jukumu jingine la TSC ni kuhakikisha Waajiri wanazingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya Serikali katika kulipa stahili, kushughulikia masuala mbalimbali ya walimu na kuiepushia Serikali madeni yasiyo ya lazima.
Akieleza zaidi, alisema kwamba TSC pia inawajibika kutenda haki katika kutoa uamuzi wa masuala ya kinidhamu na rufaa kwa walimu pamoja na kubuni namna bora zaidi ya kuwapa motisha walimu ili wafanye kazi zao kwa ufanisi.
Aliongeza kuwa, jukumu jingine ni kuelimisha walimu kuhusu masuala ya Tume, maadili, wajibu na haki za walimu katika utumishi wao.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Hape aliwaambia washiriki wa mafunzo hayo kuwa TSC ina imani na wajumbe wote wa kamati za wilaya zinazoshughulikia ajira na nidhamu kwa walimu.
“Iwapo kamati hizo zitawajibika vizuri, Tume itapunguza mzigo wa rufaa na malalamiko yanayowasilishwa na walimu,” alisisitiza.
Aidha, aliwataka wajumbe wa kamati hizo wawe huru kuhoji na kuomba ufafanuzi ili kuwa na uelewa mzuri kabla ya kutoa uamuzi wowote kwenye vikao vya kisheria.
Alisema mafunzo hayo yalilenga kuwapa ufahamu na kujiamini zaidi katika kushughulikia masuala ya walimu.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment