JAMHURI YAWAONDOLEA SHTAKA LA UTAKATISHAJI WATUMISHI WA BoT, WARUDISHWA RUMANDE | Tarimo Blog



 Na Karama Kenyunko Michuzi TV 
UPANDE wa Jamuhuri katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili watumishi nane wa Benki Kuu Tanzania (BoT) na wenzao watano imewaondolea washtakiwa, shtaka moja utakatishaji wa fedha kati ya sita yaliyokuwa yakiwakabili baada ya kuifanyia mabadiliko hati ya mashtaka.

Washtakiwa hao sasa wamebakiwa na mashtaka matano ya kuongoza genge la uharifu, kufaya uhalifu wa kupanga,  kuharibu noti, kujipatia faida kwa udanganyifu na kuisababishia Serikali hasara ya Sh 4.6 bilioni.

Mapema wakili wa serikali Mwandamizi Wankyo Simon alidai mahakamani hapo kuwa, kesi hiyo leo Juni 15, 2021 imekuja kwa ajili ya kutajwa, upelelezi bado haujakamilika, pia ameiomba mahakama kuifanyia mabadiriko hati ya mashtaka kwa ajili ya kuliondoa shtaka la utakatishaji fedha.

Hata hivyo,  hakimu mkazi mwandamizi, Godfrey Isaya anayesikiliza kesi hiyo, amewaeleza washtakiwa kuwa licha ya kuondolewa shtaka hilo la utakatishaji lakini bado mahakama ya Kisutu haina uwezo wa kuwapatia dhamana kwani kiasi cha fedha wanachoshtakiwa nacho ni kikubwa na dhamana yake inaombwa mahakama Kuu.

" Washtakiwa shtaka mnaloshtakiwa nalo bado ni ujuhumu Uchumi,  na kiwango cha pesa ni kikubwa ambacho sisi hapa hatuwezi kuwapa dhamana, mnaweza kwenda kuomba dhamana mahakama kuu, wao wakatuelekeza sisi na kutoa masharti ya dhamana", amesema hakimu Isaya.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 29, 2021 washtakiwa wote wa wamerudishwa rumande.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mariagoreth Kunzugala (29) maarufu kama Bonge, Henry Mbowe (36) maarufu kama Mzee wa Vichwa na Asha Sekiboko (30).

Wengine ni Cecilia Mpande (49), Agripina Komba (55), Zubeda Mjewa (50), Khadija Kassunsumo (57) na Mwanaheri Omqary (53) wote walikuwa wafanyakazi wa BoT na wakazi wa jijini Dar es Salaam.

Wengine ambao sio watumishi wa BoT ni Alistides Genand (44) maarufu kama Stide; Musa Chengula(39) maarufu kama Mkinga; Zaituni Chihipo(34) maarufu kama Zai na Respicius Rutabilwa(44) maarufu kama Mtashu.

Katika hati ya mashtaka inadaiwa,  kati ya Januari 2017 hadi Septemba 30 2019, washtakiwa wakiwa Watumishi wa BoT, kwa kuvunja majukumu yao ya kazi waliwezesha utendekaji wa kosa la kuongoza genge la uhalifu. 

Pia inadaiwa, Genand, Mchegage, Chengula,  Chihipo na Ishengoma wakiwa si watumishi wa BoT, kwa kushirikiana na watumishi hao wa BoT kwa makusudi, waliwezesha kutendeka kosa la uhalifu wa kupanga. 

Katika shitaka la tatu, washtakiwa wote bila ya kuwa na kibali na kutokuwa wazalendo, waliharibu noti 460,000 za Sh 10,000 kila moja kwa kuzikatakata zenye thamani ya Sh. Bilioni 4.6

Katika shtaka la nne, siku na maeneo hayo, kwa mawasilisho ya kilaghai, kwa kujua na kwa mpango wa kitapeli washtakiwa wote walijipatia faida ya Sh bilioni 1.5bilioni kutoka BoT baada ya kuwasilisha noti hizo BoT.

Katika shitaka la tano washitakiwa wote wanadaiwa kuisababishia BoT hasara ya Sh bilioni 4.6. 


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2