TANZANIA KUWA MWENYEJI WA KONGAMANO LA BIASHARA NA VIWANDA LA AFRIKA MASHARIKI | Tarimo Blog

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb.) amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda, na Wakulima Tanzania (TCCIA) Bw. Paul Koyi pamoja na Mratibu wa Kanda wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye viwanda na Wakulima Afrika Mashariki (EACCIA) Bw. Charles Kahuthu walipomtembelea ofisini kwake tarehe 16 Juni 2021 Jijini Dodoma.

Ujumbe huo unaosimamia masuala mbalimbali ya sekta binafsi ulikutana na Mhe. Balozi Mulamula kwa lengo la kuwasilisha serikalini kusudi la sekta hiyo kuipendekeza Tanzania kuwa mwenyeji wa Kongamano la Biashara na Viwanda linalotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 30 Agosti hadi 3 Septemba 2021 katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Lengo la kongamano hili ni kuziunganisha sekta binafsi ili zipate uzoefu zaidi katika masuala ya viwanda na biashara. Pia kuviandaa vyama vya biashara, viwanda na kilimo vya kanda kuwa tayari kwa ushindani wakati huu ambapo mataifa ya Afrika yanajiweka tayari kuingia katika soko huru la biashara la Afrika (CFTA).

Aidha, Rais wa TCCIA Bw. Koyi alieleza kuwa kongamano hilo litaambatana na maonesho ya bidhaa na huduma mbalimbali zinazotolewa na sekta binafsi hivyo, itakuwa ni fursa nzuri kwa sekta binafsi na wananchi kwa ujumla kushiriki katika kongamano hilo ili kujifunza masuala ya biashara na uwekezaji.

Naye mratibu wa kanda wa EACCIA, Bw. Charles Kahuthu alifafanua malengo madhubuti ya chama hicho katika kuhakikisha kongamano hilo linakuwa tofauti na makongamano mengine yaliyokwishafanyika ni pamoja na kuhakikisha kinaongeza ushirikiano na kanda nyingine ndani ya Afrika ili kuweza kufungua fursa zaidi kwa wananchi wake.

“Sisi waratibu wa sekta binafsi tumepanga Kongamano hili liwakutanishe wafanyabiashara kutoka nchi za Afrika Mashariki, nchi za Maziwa makuu, na nchi nyingine ndani ya Afrika” alisema Bw. Kahuthu

Akiongea na ujumbe huu Mhe. Balozi Mulamula ameihakikishia sekta binafsi juu ya utayari wa serikali katika kuhakikisha inafanikisha jitihada hizi zenye lengo la kuinua uchumi na kwamba itakuwa bega kwa bega kutoa ushirikiano wakati wa maandalizi na wakati wa kongamano.

Vilevile, ametoa wito kwa TCCIA kuiandaa sekta binafsi kushiriki kikamilifu kuzinadi fursa mbalimbali katika kongamano hilo. Pia akaongeza kuwa kongamano litasaidia katika kupeana uzoefu wa kukuza mitaji na masoko ya biashara nje ya mipaka ya Tanzania sambamba na kuvutia uwekezaji.

Kadhalika, ametoa wito kwa wananchi kujiandaa kutumia fursa mbalimbali zitakazopatikana kupitia ugeni huo utakaowasili nchini.

Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Afrika Mashariki (EACCIA) chenye makao yake makuu nchini Kenya ni mdau muhimu katika kusimamia masuala ya sekta binafsi ndani ya jumuiya na pia kimekuwa kikiainisha vipaumbele mbalimbali vya sekta binafsi ndani ya jumuiya kwa kushirikiana na vyama vya kitaifa vinavyosimamia sekta hiyo.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Kulia) akizungumza na Rais wa Chama cha Wafanyabiashara,Wenye Viwanda na Wakulima Tanzania (TCCIA), Bw. Paul Koyi alipomtembelea ofisini kwake tarehe 16 Juni 2021 Jijini Dodoma.Bw. Koyi alimueleza Mhe, Balozi Mulamula lengo la ujio wake pamoja na kumtambulisha Mratibu wa Kanda wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Afrika Mashariki(EACCIA) Bw. Charles Kahuthu(hayupo pichani)


Mhe. Balozi Mulamula akieleza nia ya dhati ya serikali katika kuhakikisha sekta binafsi inapewa ushirikiano ili kukuza na kuimarisha biashara ya kimataifa sambamba na uwekezaji.
Wa kwanza kushoto ni Mratibu wa Kanda wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Afrika Mashariki (CCIA) Bw. Charles Kahuthu.


Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji,Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Bernard Haule (wa kwanza kulia) akifafanua programu mbalimbali za kitaifa na kikanda zilizofanyika katika kuhamasisha sekta binafsi na umma kwa ujumla juu ya fursa zinazopatikana katika soko la Afrika Mashariki na kuwaandaa wananchi kuingia katika ushindani wa soko huru la biashara la Afrika (CFTA).


Mazungumzo yakiendelea.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2