WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameagiza korosho zote zinazozalishwa katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi zisafirishwe kupitia badari ya Mtwara kwani serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika bandari hiyo kwa kuikarabati na kuipanua.
Amesema hayo leo (Jumapili Juni 06, 2021) wakati wa kikao na wadau wa zao la korosho kilichofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Sea View, iliyopo mjini Lindi.
Amesema kuwa Rais Samia amewaagiza viongozi wa bandari wapitie tozo zote zinazowakwaza wasafirishaji ili kuwavutia kuitumia bandari hiyo "tunataka wasafirishaji watumie bandari hii kusafirisha korosho kuanzia na msimu huu".
Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa wakulima wakubali kupokea pembejeo kulingana na mahitaji yao na watalipia kulingana na idadi ya mifuko waliyochukua na sio shilingi 110 kwa kila kilo kama inavyelezwa “kila kilo ni gharama mno, lengo letu ni kuendelea kumpungumzia mzigo mkulima, msiogope kuchukua pembejeo”
Waziri Mkuu ametoa wito kwa wakulima wa zao la Korosho kuwa na utaratibu wa kubangua korosho ili kupata faida zaidi badala kuziuza bila kuzibangua "tungebangua wenyewe tungepata faida kubwa sana, wenye viwanda panueni viwanda vyenu na kukuza mitaji na wakulima wadogo endeleeni kubangua ili kuongeza thamani ya korosho zetu."
Amesema kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono wadau wote wa korosho nchini katika kufanikisha mkakati huo ikiwemo kutengeneza mashine za ubanguaji kupitia Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) "ni vyema tujikite kwenye ubanguaji kuliko kuisafirisha nje ya nchi ikiwa ghafi, tumeandaa mfumo mzuri na Rais wetu ameendelea kusisitiza katika ujenzi wa viwanda".
Akiongelea tozo ya unyaufu, Waziri Mkuu amesema kuwa tozo hiyo haikubaliki kwa kuwa haina uhalisia kwani hata sheria na kanuni kwenye Wizara ya kilimo haitambui unyaufu. "tusisikie makato ya unyaufu kwasababu yanawafanya wanunuzi wahisikuwa wanaonewa, viongozi wa Serikali tusimamie hilo, hatutaki kusikia kuhusu tozo ya unyaufu."
Vilevile Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali inaweka mpango wa kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na Afisa Ugani mmoja atakayesaidia kutoa elimu kwa wakulima juu ya namna bora ya kusimamia mazao yao ili kuongeza tija.
"wakulima wanakosa elimu ya namna ya kuliendesha zao hili, maafisa kilimo mlioko maofisini tokeni muende vijijini kuwaelimisha wakulima namna bora ya kulima mazao, wakati wote mnatakiwa kuwa shambani kuhakikisha wakulima wanalima kwa kuzingatia miongozo ya kilimo bora".
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment