MAKONGORO NYERERE AIPONGEZA SIMANJIRO KWA HATI SAFI | Tarimo Blog




Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro kwa kupata hati safi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa miaka mitatu mfululizo.

Hata hivyo, kwa muda wa miaka mitano mfululizo Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro imekuwa ikipata hati safi kwa mujibu wa taarifa ya CAG.

Akizungumza kwenye kikao cha Baraza maalum la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro ya kupokea taarifa ya CAG ya mwaka 2020, Makongoro ameipongeza halmashauri hiyo.

Makongoro amesema halmashauri hiyo imefanya jitihada kubwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali hadi kufanikisha upatikanaji wa hati safi kwa muda wa miaka mitatu mfululizo.

"Hii ndiyo wilaya yangu ya kwanza kufanya ziara tangu niteuliwe na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mkuu wa Mkoa wa Manyara, natafurahi kuwa nimeanza vizuri," amesema Makongoro.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Yefred Myenzi amesema kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020 kulikuwa na hoja 93 zilizoibuliwa na kutolewa mapendekezo.

Myenzi amesema halmashauri imefanikiwa kufunga hoja 82 baada ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa Serikali kuhakiki na kuridhia majibu yaliyowasilishwa.

Amesema hoja 11 hazijafungwa, hoja 10 za kiutendaji na hoja moja ya kimfumo ambao utekelezaji wake unaendelea kwa matarajio kuwa zitafanyiwa ufumbuzi ndani ya mwaka unaofuata.

Kaimu katibu Tawala wa mkoa wa Manyara, Kenedy Kaganda amewapongeza Simanjiro kwa kupata hati safi ila wasizalishe hoja mpya.

Kaganda amewataka viongozi wa halmashauri hiyo, kuwashirikisha wakaguzi wa ndani katika ufanyaji wa kazi zao kwani hoja nyingi huzalishwa na wakuu wa idara.

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, mhandisi Zephania Chaula amesema Halmashauri hiyo haina miradi hewa hivyo wanaomba wapatiwe watumishi wengi zaidi kwani wana uhaba wa watumishi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga Laizer amesema baada ya mafanikio hayo wataongeza zaidi ya juhudi katika kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo ili wasipate hati chafu au hati ya mashaka.

Diwani wa Kata ya Naisinyai, Taiko Kurian Laizer amesema mtumishi aliyefariki dunia ambaye alisababisha hoja moja, familia yake isamehewe deni hilo kwani hivi sasa ameshapoteza maisha.



Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2