RITA, MAHAKAMA WILAYA TEMEKE WAZINDUA KAMPENI YA HAKI MIRATHI | Tarimo Blog

Jaji Mfawidhi Lameck Mlacha akizungumza wakati wa kampeni ya Haki Mirathi iliyolenga kutoa elimu kwa jamii kuhusu sheria na taratibu zinazohusu kuandika na kuhifadhi wosia na masuala ya mirathi, Leo jijini Dar es Salaam.
Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu Bi. Emmy Hudson akitoa hotuba ya utangulizi kuhusu kuandika na kuhifadhi wosia leo jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Godwin Gondwe akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo na kueleza kuwa itasaidia hasa katika kupunguza migogoro mingi katika familia inayohusiana na masuala ya mirathi, Leo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu Dkt. Abdulrazak Badru (aliyesimama,) Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo na kueleza kuwa Serikali kupitia Bodi ya Mikopo imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa wanafunzi ambao baadhi yao wamepitia changamoto za mirathi iliyoachwa na wazazi wao. Leo jijini Dar es Salaam.







Matukio mbalimbali wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Haki Mirathi.


WAKALA wa usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) na Mahakama kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke imezindua kampeni  inayojulikana kwa jina la Haki Mirathi yenye lengo la kutoa elimu kwa jamii kuhusu sheria na taratibu zinazohusu kuandika na kuhifadhi wosia pamoja na mambo ya mirathi.  

Akizungumza hii leo Jijini Dar es salaam wakati wa ufunguzi wa kampeni hiyo Jaji Mfawidhi Mhe. Lameck Mlacha amesema kumekuwa na uelewa mdogo kuhusu sheria na taratibu za kufungua na kufunga mashauri ya mirathi sambamba na kuongezeka kwa matapeli wanaotumia mwanya huo kujitokeza kutoa msaada kwa ndugu wa marehemu na kufikia hatua ya kujimilikisha mali kinyume na warithi halali.

Mlacha ameongeza kuwa mashauri mengi yanayofunguliwa mahakamani yanachelewa kufungwa kutokana na kukithiri kwa migogoro ndani ya familia na kupelekea baadhi ya mali kupotea na hata warithi kukata tamaa ya kuendelea na mashauri hayo na kuisababishia mahakama changamoto ya mrundikano wa mashauri hayo ambapo taarifa zake huchakaa au kuharibika kabisa.

‘’Asilimia 47 ya mashauri yanayofunguliwa katika mahakama Wilaya ya Temeke yanahusu mirathi  na asilimia iliyobaki ni madai mengine, hivyo naona suluhisho pekee kwa sasa ni kuandika wosia  utakaoelezea mgawanyo wa mali zako na warithi halali badala ya kuacha ndugu waamue hatma ya mali zako mara baada ya kufariki dunia.’’Alisema  Mlacha.

Kwa upande wake Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa RITA Bi Emmy Hudson amesema kuwa jamii inapaswa kubadilika na kuachana na imani potofu iliyojengeka kwa baadhi ya watu kwa kuamini kuandika wosia ni uchuro kwakuwa jambo la kifo ni la lazima kwa kila mwanadamu hivyo ni jukumu la kila mmoja kuiandaa familia kuishi maisha bora yenye furaha mara baada ya wazazi kufariki dunia.

‘’RITA tunaandika na kuhifadhi wosia ambapo tangu mwaka 2008 wosia zipatazo 782 zimeandikwa na kuhifadhiwa sehemu salama na bado wenyewe wanaendelea kuishi bila ya hofu au imani kuwa kufanya hivyo ni uchuro, nawaomba ndugu wananchi migogoro ya mirathi suluhisho lake ni kuandika wosia na si kuwaacha ndugu waje kuamua hatima ya mali zako.’’ Alisema Bi Hudson.

Aidha Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Dkt. Abdulrazak Badru amesema kuwa Serikali imekuwa ikiwapatia mikopo baadhi ya wanafunzi  yatima ambao wazazi wao wamefariki na kuacha fedha na mali nyingi lakini kutokana na migogoro ya mirathi kwa muda mrefu inasababisha kushindwa kuwalipia gharama za masomo na kulazimika kuomba mkopo ambao ungetumika kuwasaidia watoto wengine wenye uhitaji.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Godwin Gondwe amesema kuwa kampeni hiyo inatokana na maoni na uhitaji wakati wa kampeni ya kampeni ya one stop Jawabu iliyofanyika mwaka jana wilayani humo na kuibua migogoro mingi inayotokea ndani ya familia kuhusu mirathi.

‘’Leo tumekuja na kampeni ya Haki Mirathi lengo ni kutoa elimu kuhusu  taratibu na sheria za mirathi kupitia kwa maafisa tarafa, watendaji wa kata, watendaji wa mitaa na madiwani kwa kushirikiana na RITA pamoja na mahakama wilaya ya Temeke ili kumaliza migogoro ya kugombea mali za marehemu na kusababisha mateso na vilio  kwa wajane na watoto wa marehemu.’’amesema Mhe.Gondwe.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2