Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili akikagua moja ya lori lililokamatwa na shehena ya maharage ambayo yanadaiwa kutolipiwa ushuru.
Mkaguzi wa mazao katika Kituo cha Njia Panda, Juma Athumani akitoa maelezo kwa DC Muragili jinsi alivyo yakamata magari hayo.
Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Hassan Ngoma (katikati) akizungumzia tukio hilo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
SERIKALI mkoani Singida imekamata malori matano yenye magunia ya mazao mchanganyiko zaidi ya tani 40 yaliyokuwa yakipitia mkoani hapa bila ya kuwa na nyaraka zozote za kulipia ushuru.
Kufuatia kukamatwa kwa shehena hiyo Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili aliagiza Wafanyabiashara hao waliokuwa wakisafirisha shehena hiyo ya mazao kutozwa faini ya sh.milioni 4.5 ukiwemo ushuru.
"Faini kwa Mfanyabiashara wa maharagwe, Philipp Lehema ni sh.milioni 4 na mwenzake Moses Zelothe ni sh.500,000." alisema Mulagiri.
Akifafanuaa kuhusu faini hizo Mulagiri alisema kwa kosa la kudanganya kuhusu ulipaji huo Lehema alitozwa faini ya sh.200,000 kwa kila gari kati ya manne yaliyokuwa na mzigo huo na kutakiwa kulipa ushuru wa sh.3000 kwa magunia 1200.
Alisema kwa mfanyabiashara Zelothe alitozwa faini ya sh. 200,000 kwa gari lake na sh. 300,000 kwa magunia 150 ya mchele ambayo hakuyalipia ushuru.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Muragili alisema shehena hiyo ya mazao aina ya maharage na mchele ilikuwa ikisafirishwa kutoka mkoani Kagera na Tabora kwenda Arusha.
Alisema shehena hiyo ilikamatwa ikisafirishwa kwenye malori matano, manne yenye maharage yakiwa ya Lehema na lenye pumba na mchele likiwa la Zelothe.
Alitaja namba za malori hayo kuwa ni T 335 AWH, T 178 CBB, T 662 DTL, T 489 DUV na T 850 AFQ.
Alisema wafanyabiashara waliokamatwa wakisafirisha shehena hiyo walikuwa wakitumia stakabadhi za malipo ya maegesho ya magari wakati wakipakia mazao hayo kukwepa ushuru.
Mfanyabiashara Philipp Lehema ambaye alikuwa akisafirisha maharage hayo alikiri kusafirisha bidhaa hiyo kwa kutumia stakabadhi ya ushuru wa maegesho na ameshangaa kuona akikamatwa kwa madai ya kutolipa ushuru wakati yeye alifahamu ameshalipia ushuru huo kwa kutumia stakabadhi hizo.
Muragili alitumia nafasi hiyo kutoa onyo kwa wafanyabiashara wenye tabia ya kukwepa kulipa ushuru kwa visingizio mbalimbali na kwamba kwa Mkoa wa Singida hawatapita watakamatwa.
Mkaguzi wa mazao katika Kituo hicho cha Njia Panda kilochopo wilayani humo, Juma Athumani alisema baada ya kuyakamata magari hayo wahusika wenye mzigo huo walijaribu kumshawishi hayaruhusu magari hayo lakini aliwakatalia kwa kuwa alijua kufanya hivyo ilikuwa ni kuikosesha Serikali mapato.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Rashid Mandoa amempongeza mkaguzi huyo na wenzake waliokuwa zamu siku hiyo kwa kuwa na moyo wa kizalendo na ameahidi kuwapa motisha.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment