Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
TAASISI ya Wajibu imesema kwamba imepitia na kuchambua Bajeti ya Serikali ya mwaka 2021/2022 ambapo kwa sehemu kubwa wameipongeza kwa kuja na vyanzo vipya vya ukusanyaji mapato ikilinganishwa na bajeti za miaka iliyopita.
Akizungumza leo Juni 16,2021, kuhusu uchambuzi wa bajeti ya Serikali, Mkurugenzi Mtendaji wa Wajibu Ludovick Utouh amesema taasisi hiyo aliianzisha mwaka 2015 ikiwa na malengo ya kujenga uwezo wa wananchi kufahamu mambo yanayowahusu uwajibikaji wa rasilimali za Taifa.
"Sisi wajibu tunajikita zaidi kwenye uwajibikaji kwenye rasilimali za taifa,niseme ni mara ya kwanza leo WAJIBU imeingia kwenye kuchambua bajeti ya Taifa kwa jicho la uwajibikaji.Tunafahamu Juni 10 mwaka huu Waziri wa Fedha na Mipango Dk.Mwigulu Nchemba aliwasilisha bajeti ya Serikali bungeni.
"Ni bajeti ya mwaka 2021/2022 ni bajeti ya kwanza chini ya mpango wa tatu wa maendeleo ya taifa wa miaka mitano na ni bajeti ya kwanza pia kwa awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan na bajeti hii na mpango huu inachukua dhima inayosema kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu,"amesema Utouh.
Amefafanua taasisi ya Wajibu imefanya uchambuzi wa bajeti pendekezwa kwa kuzingatia uwazi, uwajibikaji na utawala bora, hivyo imekuja na maoni, changamoto na mapendekezo yanayolenga kuboresha ukamilishaji wa bajeti ya taifa ya mwaka 2021/2022.
"Kama tulivyoona na tulivyosoma , makadirio ya bajeti ya Serikali ya mapato na matumizi yameweka malengo ya jumla kwa kuanza na lengo la kwanza la kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara kwa kuweka mazingira rafiki kwa mlipa kodi.
"Kwa lengo la kuvutia uwekezaji, ukuaji wa biashara ndogondogo na zakati ili kapunia wigo wa kodi.Pili kuboresha mifumo ya usimamizi na ukusanyaji wa kodi ili kupanua wigo wa kodi.Kwa kweli bajeti hii imekuja na vyanzo vipya vya mapato ya Serikali ambavyo huko nyuma havijakuwepo.
"Zamani mabajeti mengi ya Serikali yakuliwa ni marudio ya yaliyofanyika huko nyuma, lakini safari hii tunaona Serikali imekuja na taratibu za kukusanya mapato kwa kutumia ufumo wa ununuzi wa umeme LUKU, mfumo ambao hakuwepo nyuma.
"Wamekuja kwenye kodi ya laini za simu ambayo ni kitu kipya na vile vile Waziri ametuambia Serikali inaingia kwenye hati fungani za manispaa kama njia ya mapato ya Serikali, tunapaswa kuipongeza Serikali kwa ubunifu huo,"amesema.
Ameongeza pia bajeti inalenga kuimarisha uendeshaji wa mashirika ya umma ili kuendelea kufanya kazi kibiashara, kuongeza uzalishaji wa mazao yatokanayo na sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.Pia kuboresha kilimo cha umwagiliaji, kuogeza mnyororo wa thamani na masoko ya mazao ya kilimo, kuchochea uvumbuzi na uhuhishaji wa teknolojia kutoka nje.
"Kuchochea uwekezaji kwenye viwanda hasa zinazotumia malighafi zinazotoka hapa nchini, kudhibiti utoroshaji madini na kujenga mitambo ya uchenjuaji madini nchini pamoja na viwanda vya kuongeza thamani kwenye madini yanayozalishwa nchini.
"Ikiwemo jitihada za maksudi za kuwajengea uwezo zaidi wachimbaji wadogo katika ushiriki wao sekta hii, uboreshaji wa miundombinu ya sekta ya usafirishaji wa nishati , kuboresha utoaji huduma za kijamii hasa katika sekta ya afya,elimu na maji.
"Na kuimarisha ushirikiano wa nchi yetu na nchi jirani,kanda na kimataifa. Haya ndio malengo makuu ya bajeti inayozungumziwa sasa hivi bungeni.Hivyo uchambuzi wa bajeti hii tuliofanya tumeona kuna masuala matano ambayo bajeti imeyataja, ukweli ukienda kwenye ripoti za CAG za miaka ya nyuma zilikuwa ni mapendekezo.
"Kwa ajili ya utekelezaji wa Serikali, nitaeleza mabadiliko ya sheria ya ukaguzi wa umma sura ya 418, kama mtakumbuka mwaka 2013 Serikali ilileta mabadiliko ya sheria ya ukaguzi ya mwaka 2008 ambapo sheria ilitaka CAG anawapasilisha ripoti zake bungeni kama alivyowasilisha Aprili mwaka huu, serikali nayo inatakiwa kwenda sambamba siku hiyo hiyo iwasilishe majibu,"amesema.
Ameongeza hiyo kitu ilipingwa sana lakini ilipita, hivyo kwa wao watalaamu wa ukaguzi walijua haitekelezeki.Bahati nzuri Serikali imetambua hilo na imekuja na mapendekezo ya kubadilisha yale marekebisho yaliyofanyika mwaka 2013 .
"Pili kuna mabadiliko ya sheria ya mikopo , dhamana na misaada sura ya 134, nayo hii mabadiliko haya yatairusu Serikali kuidhamini kampuni au taasisi yoyote ya umma kukopa kiasi kisichozidi hisa za serikali au taasis husika.
"Ambapo hii inaenda kujibu pendekezo la CAG ambapo amekuwa anahoji mara nyingi kuhusu upungufu wa mitaji kwa mashirika yanayosimamiwa na Serikali .Tatu kuna kumekuwa na kelele kuhusu mikopo ya Serikali kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
"Ukweli Serikali inakopa hailipi na wakati mwingine hailipi riba , kwa hiyo mara nyingi inapochukua miaka mingi kwa kulipa madeni yale inaathiri utendaji kazi wa mifuko hiyo.Kwa hiyo bajeti hii inatuambia Serikali italipa madeni inayodaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kutenga fedha kwenye bajeti na kutumia hatifungani zitakazoiva kwa nyakati tofauti kuanzia miaka miwili hadi miaka 25.
"Hii itasaidia kuyajumuisha madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii kwenye deni la taifa, mara nyingi madeni hayo yalikuwa hayaingizwi kwenye deni la taita.Utaratibu huo sasa madeni hayo yatakuwa yanaingizwa kwenye deni la taifa, itasaidia mifuko hii kuwa na fedha za kuwekeza na kujiendesha kwa ufanisi zaidi,"amesema.
Aidha amesema jambo la nne katika baheri hiyo ni Serikali kuongeza mapambano zaidi dhidi ya rushwa, udanganyifu na ubadhirifu wa mali za umma."Kama mnavyojua ile lugha ya ufisadi huko nyuma , pesa kupigwa huko na huko kitu ambacho CAG amekuwa akikizungumza kila wakati.
"Serikali kusema kweli imedhamiria kukaza uzi , na kuweka mazingira magumu zaidi ya upotevu au matumizi mabaya ya fedha na serikali za taifa. Kuna mfano wa mwenendo wa fedha na makusanyo ya serikali yenye viashiria vya rushwa kwa miaka mitatu iliyopita.
"Na tano ni mapato ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) na Wakala wa Meli Tanzania(TASAC) kuanzia mwaka 2021/2022 yatakusanywa na mfumo huo kupitia GPE na kuingizwa kwenye akaunti ya makusanyo zilizopo Benki Kuu.
"Nafikiri hizi zimetokana na maoni ya CAG kwenye ripoti yake ya mwaka 2019 ambapo kuliokana kuna upotevu Sh.bilioni 3.9 kutokana na udanganyifu katika Bandari ya Kigoma na Mwanza ambao ulitokana na udhaifu wa mifumo ya ndani katika usimamizi wa malipo, hivi kwa upande wa CAG ni furaha, tunaona utekelezaji wa mapendekezo yake.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe tawi la Dar es Salaam Profesa Honest Ngowi amesema bajeti ya mwaka huu kuna aina mpya za ukusanyaji kodi ambazo zinaweza kuwa na mjadala kwa mfano kutoza kupitia umeme ina mjadala wake lakini ni aina tofauti ya kutoza hiyo kodi ukilinganisha na ilivyozoeleka.
"Njia ya kwanza ni kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara , hapo ndipo tunapozungumzia wigo wa kupanua kodi, na hii muhimu kwasababu kodi zote hizi zinatokana na uzalishaji wa bidhaa na huduma usipopanua wigo na uwekezaji zaidi utazikosa.
"Lakini kuboresha mazingira yatakayochochea ulipaji kodi wa hiyari, hiyo muhimu sana.Ulipaji kodi wa kushurutishana ni gharama sana na unaweza kuangukia fedha nyingi kupotea lakini utumiaji wa TEHAMA unarahisisha ukusanyaji wa kodi.
"Siku hizi kuna mfumo wa kulipia kodi zako kiganjani, msingi wake kuna watu wanataka kulipa kodi lakini kwenda kupanga foleni kwenye mabenki inapoteza muda lakini kufanya kiganjani ndio kinazungumziwa hapa,"amesema Prof.Ngowi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya WAJIBU , Ludovick Utouh akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari leo mkoani Dar es Salaam kuhusu uchambuzi wa bajeti ya Serikali,ambapo Taasisi ya WAJIBU imesema kuwa imepitia na kuchambua Bajeti ya Serikali ya mwaka 2021/2022 na kwamba sehemu kubwa wameipongeza kwa kuja na vyanzo vipya vya ukusanyaji mapato ikilinganishwa na bajeti za miaka iliyopita,Pichani kulia ni Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe tawi la Dar es Salaam Profesa Honest Ngowi .
Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe tawi la Dar es Salaam Profesa Honest Ngowi akifafanua jambo mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo mkoani Dar es Salaam,wakati akifafanua kuhusu Bajeti ya Mwaka huu na uwepo wa aina mpya za ukusanyaji kodi tofauti na ilivyozoeleka hapo awali
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment