CHETI CHA DAWA KILICHOBORESHWA KUANZA KUTUMIKA JULAI 10 | Tarimo Blog


Na. WAMJW-Dar es Salaam.

Wataalamu wa afya wakiwemo waandishi wa dawa (Prescribers) na watoa dawa (Dispenser) katika vituo vyote  vya umma ngazi zote za kutolea  huduma za afya nchini  wametakiwa kuandika na kutoa dawa kwa kutumia  cheti cha dawa (Prescription) iliyoboresha  kuanzia tarehe 10 Julai, 2021.

Rai hiyo imetolewa leo na Mfamasia Mkuu wa Serikali kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw. Daudi Msasi wakati akitoa tamko la matumizi ya cheti cha dawa (Prescription) kwa ngazi zote za kutolea huduma za afya nchini kwenye ukumbi wa Bohari ya Dawa (MSD) jijini Dar es Salaam.

Bw. Msasi amesema kuwa cheti hicho cha dawa itawezesha kuwa na kumbukumbu sahihi za matumizi ya dawa na pia kurahisisha ufuatiliaji wake na kupata ushahidi na katika maboresho  ya kitabu hicho waliyofanya wametengeneza nakala tatu  ili kuweza kusaidia  kulinganisha kilichoandikwa na mtaalam,aliyetoa dawa au mtumiaji aliyepewa bidhaa za afya hivyo siku wakitaka kuhakiki iwe rahisi.

“kutokana na umuhimu wa kufahamu watumiaji wa bidhaa za afya na uwezekano wa kupata ushahidi kutoka kwao juu ya dawa walizopewa, wizara imefanya maboresho kwenye cheti cha daktari kwa kuongeza baadhi ya taarifa ikiwepo namba ya simu ya mgonjwa aliyepewa dawa, jina na cheo cha mtoaji dawa na pia kuanisha kama dawa zilitolewa bure (msamaha) au zililipiwa au zitalipwa na Bima ya Afya”. Alisisitiza Bw. Msasi.

Aliongeza kuwa tayari Bohari ya Dawa (MSD) imeshachapisha vitabu vipatavyo 65,000,000 na ameelekeza MSD kuanza kusambaza na kufikisha kwenye kanda zao nchi nzima ili vituo vya afya waanze kuvitumia na pale wanapoishiwa wanatakiwa kupakua kwenye tovuti ya kwani Wizara tayari imeshakipakia cheti hicho.

Amesema kufuatia kaguzi za dawa zilizofanywa na Wizara ya Afya katika ngazi za Hospitali za Halmashauri na za Rufaa za Mikoa, kulibainika upungufu katika maeneo zaidi ya kumi na sita  yenye kuashiria usimamizi hafifu wa bidhaa za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

“Sehemu kubwa ya upungufu huo ni kutotumia ipasavyo miongozo na nyezo muhimu katika utunzaji na utoaji wa bidhaa za afya nchini zilizoandaliwa na kutolewa na Wizara ya Afya”.Alisema Bw. Msasi.

Alitaja  miongozo hiyo ni pamoja na Muongozo wa matibabu  nchini (STG) ambao umekuwa na dawa unaotumika kutibu wananchi wa Tanzania katika utoaji wa huduma za dawa nchini ambao unasimamia  eneo zima la fedha lakini eneo la ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.

“Kwenye huu muongozo tumeeleza ni dawa gani zitumike kutibu ugonjwa wa namna gani nchini na kutumika katika ngazi zote hadi hospitali ya Taifa,mfano kama una presha unapewa dawa ipi kumtibu mgonjwa na kama itashindikana ni dawa ipi iendane na kama itashindikana tumeandika mpaka dawa ya tatu, pia ngazi za dawa zitumike kuanzia Zahanati, Wilaya, Mikoa na Taifa kwahiyo kuna kundi A, B, C, D na S (kundi S ni kwa ajili ya magonjwa makubwa ambazo zinatolewa na madaktari bingwa)”. Alifafanua Bw. Msasi

Alisisitiza wataalam hao lazima kuzingatia muongozo huo ili kutomsumbua mgonjwa kutokupata dawa endapo atakua ameenda kutibiwa mfano kwenye zahanati lakini akaandikiwa dawa ambazo zipo kwenye kundi la kutolewa na madaktari bingwa,pia dawa zilizopo ni zile zenye majina halisi (generic) na sio majina ya kibiashara ambapo inapelekea wananchi kukosa dawa au kununua kwa bei kubwa zaidi.

Bw. Msasi alisema Muongozo  wa kamati ya Dawa na Tiba ambao unawapa maelekezo wasimamizi namna ya kununua au kufuata dawa kwenye kituo kingine ili wachukue hatua zipi na kumpa nafasi Mganga Mfawidhi kufuata na hivyo una muongozo wa matumizi sahihi ya bidhaa za afya zikiwemo dawa na vifaa tiba pia inashauriana namna ya kuandika dawa kupitia muongozo wa matibabu na kuweza kusimamia bidhaa za dawa kwenye vituo vya afya.

Mfamasia Mkuu wa Serikali amesema kutokana na sababu mbalimbali zimekua zikitolewa na wasimamizi  au watendaji wa vituo  hivyo  vya umma juu ya kukosekana  kwa miongozo au nyenzo hizo hivyo Wizara  kwa kutambua hilo imeweka  miongozo na nyezo hizo kwenye tovuti ya wizara hiyo.






Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2