HALMASHAURI YA MADABA KINARA MIKOPO YA MAKUNDI MAALUM | Tarimo Blog

Na Muhidin Amri,Madaba

HALMASHAURI ya wilaya Madaba mkoani Ruvuma, imetoa jumla ya Sh.87,000,000 sawa na asilimia 100 kama mikopo isiokuwa na riba kwa makundi maalum ya vijana,wanawake na walemavu kwa mwaka wa fedha ulioishia Mwezi Juni 2021.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Shafi Mpenda amesema hayo katika hafla fupi ya kukabidhi vyeti kwa viongozi wa vikundi vya kijamii vilivyofanikiwa kusajiliwa kwa njia ya mfumo mpya wa mtandao(Online).

Mpenda amesema,mwaka wa fedha 2019/2020 Halmashauri kupitia mapato yake ya ndani ilitoa kiasi cha Sh.30,000,000 kati ya hizo vikundi 12 vya wanawake vilipata Sh.25,300,000, kikundi 1 cha vijana Sh.3,000,000 na kikundi 1 cha walemavu kilipata Sh.2,000,000.

Amesema, kwa mwaka wa fedha 2020/2021 Halmashauri iliweka lengo la kutoa mikopo ya Sh,74,000,000 hata hivyo, wamefanikiwa kutoa Sh. milioni 87 kati ya hizo wanawake wamepata Sh.58,338,000,vijana Sh 19 na walemavu wamepata Sh.10.

Kwa mujibu wa Mpenda, hayo ni mafanikio makubwa kupatikana tangu Halmashauri ya Madaba ilipoanzishwa rasmi mwaka 2015 na wataendelea kuboresha kiwango cha mikopo kadri Halmashauri itakavyofanya vizuri kwenye makusanyo yake ya ndani.

Aidha amesema, Halmashauri imeanza kufanya utambuzi rasmi wa vikundi 123 vya kijamii vilivyosajiliwa kwa mfumo wa mtandao na utekelezaji wa maagizo ya Serikali kama Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inavyotakaza.

Amesema,hatua hiyo imesaidia kuongeza mahusiano kati ya ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri na wana vikundi wenyewe ambao kupitia hafla hiyo watafahamu wapi pa kwenda pindi wanapohitaji mikopo au huduma nyingine ambazo zinahitaji ushauri na msaada wa wataalam.

Mpenda ameeleza kuwa,lengo la kukutana na wana vikundi lina lenga kufahamiana, kutengeneza mkakati na utaratibu mzuri utakaosaidia kuboresha vikundi hivyo kupitia idara ya maendeleo ya jamii na namna wana vikundi wanavyoweza kupata elimu juu ya kuendesha vikundi.

Amesema,Halmashauri ya wilaya Madaba itaendelea kutoa ushirikiano kwa wanananchi ili vikundi vinavyoanzishwa na kuibuliwa ili viwe na tija na viwasaidie kuboresha maisha yao kupitia miradi husika, na kuitumia ofisi ya Mkurugenzi na wataalam waliopo kupata huduma bora na kutoa taarifa pale wanapoona kuna changamoto katika uendeshaji wa vikundi vyao.

Kwa upande wake Afisa maendeleo ya jamii msaidizi wa Halmashauri hiyo Bashiru Mgwasa amesema,jumla ya vikundi 114 vimesajiliwa kati ya hivyo vya wanawake 48,vijana 16 watu wa kundi maalum 8 na mchanganyiko 42.

Mgwasa amesema, jumla ya wanachama waliosajiliwa kupitia vikundi hivyo ni 1680 kati yao wanaume 443,wanawake 1237 na vikundi hivyo vinatoka katika vijiji 22 vilivyopo katika kata zote 8 za Halmashauri ya wilaya Madaba.

Amesema, kwa kuwa vikundi hivyo vinajishughulisha na masuala ya fedha na vinatoa fursa kwa watu kujiendesha kiuchumi,ni muhimu kuwa na kanuni na taratibu za namna bora ya kujiendesha kwa kuzingatia misingi ya utawala bora ikiwemo uwazi na uwajibikaji katika vikundi.

Hata hivyo amesema, changamoto kubwa ni baadhi ya maeneo katika kuna tatizo la upatikanaji wa mtandao(Network) kama Mateteleka,Ngadinda,Maweso,Ifinga na Igawisenga jambo lililosababisha vikundi vilivyopo katika maeneo hayo kutosajiiwa kwa mfumo wa mtandao.

Kwa upande Mwenyekiti wa Halmashauri ya Madaba Theofanes Mlelwa amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Shafi Mpenda kwa kusimamia vizuri suala la mikopo kwa makundi ya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu.

Hata hivyo,ameagiza Idara ya maendeleo ya jamii kuendelea kuvitambua vikundi katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na kutoa mikopo kwa wananchi hasa wenye mahitaji maalum ili waweze kujitegemea na kuondokana na umaskini..

Afisa Maendeleo ya jamii wa Halmashauri ya wilaya Madaba Anitha Makota kulia akimkabidhi cheti cha shukurani  jana Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Theofanes Mlelwa katika hafla fupi ya kukabidhi vyeti kwa vikundi 114 vya kijamii katika Halmashauri hiyo,katikati ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Shafi Mpenda.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri  ya Madaba mkoani Ruvuma Shafi Mpenda kushoto, akipokea cheti maalum kutoka kwa  Afisa Maendeleo ya jamii  wa Halmashauri hiyo Anitha Makota,kutokana na kutambua mchango wa ofisi ya Mkurugenzi kwa idara hiyo kutoa mikopo ya Shilingi milioni 87 sawa  na asilimia 100 kwa vikundi vya wanawake,vijana na walemavu katika Halmashauri hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Madaba Shafi Mpenda,Mwenyekiti wa Halmashauri  Theofanes Mlelwa na baadhi ya madiwani wakiwa katika picha ya  pamoja na wanakikundi  kutoka kijiji cha Mkongotema,kulia Afisa maendeleo ya Jamii Anitha Makota.
Baadhi ya viongozi wa vikundi mbalimbali vya kijamii katika Halmashauri ya Madaba wakifurahi sambamba na viongozi wa Halmashauri ya Madaba wilayani Songea wakati wa  hafla fupi ya kukabidhi vyeti iliyofanyika katika Ofisi za Halmashauri Madaba


 


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2