Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Wakili Stephen Byabato ameielekeza TANESCO ifikapo tarehe 15 Agost, 2021 umeme uwe umefika kwenye kituo cha Afya cha Nyaruyoba kilichopo wilayani Kibondo mkoani Kigoma.
Naibu Waziri Byabato ameyasema hayo kufuatia maelekezo ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Philip Isdor Mpango alipokuwa katika ziara ya kikazi mkoani Kigoma tarehe 17 Julai, 2021 mara baada ya kuzindua Kituo cha Afya cha Nyaruyoba.
Awali, Mkurugenzi wa Halmshauri ya Kibondo alimueleza Makamu wa Rais kuhusu changamoto wanazokutana nazo kuhusiana na kukosekana kwa umeme katika kituo cha Afya cha Nyaruyoba na kuomba kupatiwa umeme katika kituo hicho.
Naibu Waziri Byabato, amewaambia wananchi wa Nyaruyoba kuwa, gharama za kuunganishiwa umeme ni shilingi 27,000 tu na kuwa hakuna kuuziwa nguzo wala transforma.
Aidha, Naibu Waziri Byabato ameiagiza TANESCO ifungue ofisi ya malipo Nyaruyoba ili kuwapunguzia wananchi kwenda umbali mrefu kulipia gharama za kuunganishiwa umeme.
Pia, Naibu Waziri Byabato amesema ifikapo Oktoba 2022, Grid ya Taifa itakuwa imefika Kigoma na kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme.
Ameongeza kuwa, vijiji vyote ambavyo havijaunganishiwa umeme wilayani Kibondo na Kigoma kwa ujumla vitakuwa vimepatiwa umeme ifikapo mwezi Desemba 2022.
Naibu Waziri Byabato, amewataka TANESCO waendelee kuwaunganishia umeme wateja ambao bado hawajaunganishiwa umeme wakati wa Mradi.
Vile vile akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa jengo la Halmashauri ya mji wa Kasulu uliofanywa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango tarehe 17 Julai, 2021, Naibu Waziri Byabato ameielekeza TANESCO kuongeza jitihada za kufunga mashine moja ya MW 1.25 ili kuboresha zaidi upatikanaji wa umeme wilayani Kasulu.
Malekezo ya Naibu Waziri ni kutokana na maelezo ya Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini aliyomweleza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Philip Isdor Mpango kuhusu changamoto za upatikanaji wa umeme katika wilaya ya Kasulu.
Naibu Waziri Byabato ameshiriki katika ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia tarehe 15 Julai hadi 18 Julai, 2021 Mkoani kigoma.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment